NA DENIS MLOWE,IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amezindua rasmi bonanza kubwa la watumishi lililofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa, akisisitiza umuhimu wa umoja, mshikamano na kuimarisha afya kwa watumishi wa sekta za umma na binafsi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema bonanza hilo lina malengo makuu matatu ambayo ni kuwaleta pamoja watumishi, kuimarisha afya kupitia michezo, na kujenga mshikamano katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alieleza kuwa tukio hilo limekuwa jukwaa muhimu la watumishi kuonyesha vipaji vyao nje ya mazingira ya kazi za kila siku.
“Leo tumepata nafasi ya kuona vipaji vipya kwa watumishi wetu, ambao mara nyingi tunawaona katika majukumu ya ofisini. Hii inaonyesha kuwa kuna fursa kubwa ya kuendeleza vipaji na hata kuwasaidia kujipatia kipato kupitia michezo na sanaa,” alisema.
Aidha, aliwataka wakuu wa taasisi, mashirika na makampuni kuanzisha na kuendeleza matamasha ya michezo katika maeneo yao ya kazi ili kuimarisha afya za watumishi na kukuza vipaji.
Alisisitiza kuwa uongozi wa mkoa uko tayari kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kufanikisha shughuli hizo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa sekta binafsi kuendelea kudhamini matukio ya michezo na burudani, akieleza kuwa uwekezaji katika maeneo hayo huleta manufaa ya kijamii na kiuchumi kwa jamii.
“Udhamini wa matamasha kama haya si hasara, bali ni uwekezaji wenye matokeo chanya kwa jamii na taasisi husika,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mratibu wa bonanza hilo, Ramadhani Rashidi Shemhiru, alisema tukio hilo limehusisha zaidi ya taasisi 30 kutoka ndani ya mkoa huo, likiwa na michezo zaidi ya 17 ikiwemo mpira wa miguu, netiboli, mpira wa kikapu, voliboli, pamoja na michezo ya jadi kama kuvuta kamba na kukimbiza kuku.
Alisema lengo kuu la bonanza hilo ni kuwakutanisha watumishi wa sekta ya umma na binafsi ambao mara nyingi hawapati fursa ya kukutana, pamoja na kuimarisha afya na kujenga ushirikiano.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, alisema bonanza hilo limekuwa chachu ya kuimarisha mahusiano baina ya watumishi na kuongeza ari ya kufanya kazi kwa pamoja.
Alibainisha kuwa pamoja na michezo, tukio hilo limeambatana na burudani mbalimbali zitakazoendelea hadi usiku.
Kwa ujumla, bonanza hilo limeelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuendeleza mshikamano, afya bora na maendeleo ya kijamii miongoni mwa watumishi wa Mkoa wa Iringa.





