Mfamasia kutoka Kitengo cha Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini katika Bohari ya Dawa (MSD), Bwiro Magesa, amewasilisha mada kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo wakati wa semina kati ya MSD na wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika katika ghala kuu la MSD Kizota jijini Dodoma.
Amesema MSD imeendelea kutumia teknolojia za kisasa ikiwa ni pamoja na mifumo ya Tehama kuboresha utendaji wake, sambamba na kuimarisha vituo vyake vya usambazaji vinavyochangia ongezeko la mapato ya taasisi hiyo.
Bwiro ameeleza kuwa mapato ya MSD yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka shilingi bilioni 315 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 640 mwaka uliopita, jambo linaloonesha ukuaji wa taasisi hiyo.
Amefafanua kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo serikali, taasisi za dini na wadau wengine wa maendeleo wanaochangia kuimarisha sekta ya afya.
Aidha, amesema kuongezeka kwa imani ya vituo vya kutolea huduma za afya kumeifanya MSD kuweza kuuza bidhaa zake hata kwa kutumia mapato ya ndani ya vituo hivyo, mbali na fedha zinazotolewa na serikali.
Ameeleza kuwa MSD inafanya kazi kwa mfumo wa mtaji unaozungushwa (capital revolving), ambapo mtaji uliotolewa awali hutumika kununua bidhaa na kurejeshwa kupitia mauzo ili kuendeleza mnyororo wa ugavi.
Kwa mujibu wa Bwiro, upatikanaji wa bidhaa za afya umeongezeka kutoka asilimia 42 miaka minne iliyopita hadi kufikia asilimia 73 kufikia Machi mwaka huu, huku lengo likiwa kufikia asilimia 100.
Ameongeza kuwa vituo vya afya vinavyosimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI vimeongeza kiwango cha utimizaji wa mahitaji kutoka wastani wa asilimia 41 hadi kufikia zaidi ya asilimia 70, hali inayodhihirisha kuimarika kwa huduma.
Katika kuboresha huduma, amesema MSD imefanikiwa kupunguza gharama za baadhi ya bidhaa kupitia ununuzi wa kimkakati kutoka kwa wazalishaji, ambapo bei imepungua kutoka takribani shilingi 179,000 hadi 70,000 kwa baadhi ya vifaa.
Amebainisha kuwa taasisi hiyo pia imewekeza katika miradi ya kimkakati ikiwemo huduma za mama na mtoto, afya ya meno na vifaa maalum vya matibabu ambavyo hapo awali vilikuwa vigumu kupatikana.
Kuhusu miundombinu, Bwiro amesema MSD inaendelea kuboresha maghala yake, ikiwemo ghala la Dodoma pamoja na ujenzi wa ghala jipya Chato, ili kuongeza ufanisi wa uhifadhi na usambazaji wa bidhaa.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo inapanga kutumia nishati mbadala kama sola pamoja na magari ya kisasa yanayotumia umeme na mafuta ili kupunguza gharama za uendeshaji na kulinda mazingira.
Hata hivyo, ameeleza kuwa MSD inakabiliwa na changamoto ikiwemo uhaba wa mtaji, madeni kutoka kwa vituo vya afya na utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Amehitimisha kwa kuwataka wanahabari kushirikiana na MSD katika kutoa elimu sahihi kwa umma kuhusu upatikanaji wa dawa na huduma za afya, pamoja na kupambana na taarifa potofu ili kuboresha sekta hiyo nchini.





