Na Happy Lazaro, Arusha
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka viongozi wa serikali za mitaa nchini kuachana na migogoro ya ndani inayokwamisha maendeleo, akisisitiza kuwa ni wakati wa kujikita katika wa miradi yenye tija kwa wananchi.
utekelezaji.
Akifungua Mkutano Mkuu Maalumu wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika jijini Arusha, Dkt. Nchemba amesema migogoro ya mara kwa mara ndani ya halmashauri imekuwa ikichelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, jambo lisilokubalika.
Amesema baadhi ya migogoro hiyo inachochewa na utaratibu wa uchaguzi wa kila mwaka wa baadhi ya nafasi za uongozi, hususan makamu wenyeviti, hali inayosababisha makundi pinzani na ushindani usio na tija.
“Kila mwaka kunakuwa na uchaguzi, wanaoshindwa wanaunda makundi yao na kuanza kupambana na walioshinda. Badala ya kufanya kazi, viongozi wanajikuta wapo kwenye kampeni zisizoisha,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu ameelekeza kufanyika mapitio ya utaratibu huo ili kupunguza migogoro. Alisema iwapo changamoto hiyo ipo kisheria, basi hatua zichukuliwe kurekebisha sheria au kanuni husika ili kuweka mfumo utakaosaidia kuimarisha utulivu na ufanisi wa uongozi.
Ameongeza kuwa migawanyiko ndani ya mabaraza ya madiwani imekuwa ikiwapa wakati mgumu wenyeviti na mameya kuendesha vikao na kusimamia maendeleo, kutokana na presha ya makundi ya kisiasa ndani ya halmashauri.
Katika hatua nyingine, Dkt. Nchemba amewataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanachagua viongozi wenye sifa ya uzalendo, uwajibikaji na wanaopinga rushwa kwa vitendo, ili kuimarisha utendaji na kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Tunahitaji viongozi watakaoacha alama, watakaoleta mabadiliko na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati,” amesisitiza.
Aidha, amewataka viongozi kuwa wabunifu katika kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuvutia uwekezaji, akibainisha kuwa dunia inabadilika na haiwezekani kuendelea kutegemea mifumo ya zamani.
Akizungumzia uchumi, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kukuza sekta binafsi kama nguzo ya maendeleo, akieleza kuwa haiwezekani kuongeza mapato bila kuiwezesha sekta hiyo kukua.
Ametumia mfano wa jamii za wafugaji kueleza umuhimu wa kulea rasilimali kabla ya kunufaika nayo, akisema viongozi wanapaswa kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi ili iweze kuchangia kikamilifu katika ustawi wa taifa.
Mkutano huo wa ALAT unatarajiwa kuchagua viongozi wapya watakaosimamia jumuiya hiyo katika kipindi kijacho, huku matarajio yakiwa ni kupata uongozi utakaosaidia kuimarisha utendaji wa serikali za mitaa nchini.





