NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini,Fadhili Ngajilo ameibua hoja kuhusu hatima ya ujenzi wa barabara muhimu inayounganisha Pawaga na Iringa Mjini, akisisitiza umuhimu wake katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi, hususan katika eneo la Pawaga ambako serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni sita kwa ajili ya mradi wa uzalishaji chumvi.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni, mbunge huyo alieleza kuwa hadi sasa ni kilomita 20 pekee za barabara hiyo ndizo zimepata kibali cha kujengwa tangu mwaka wa fedha 2020, huku kilomita 41 zilizobaki zikipita katika maeneo ya jimbo lake, yakiwemo maeneo ya Ilala na Mkwawa.
Mbunge Ngajilo alitaka kufahamu ni lini serikali itaanza ujenzi wa sehemu iliyosalia ili kuhakikisha barabara hiyo inakamilika na kuleta tija kwa wananchi na uwekezaji uliofanyika.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi mhandisi Godfrey Kasekenya alieleza kuwa serikali ina mpango wa kuanza na ujenzi wa kilomita 20 za awali kwa kiwango cha lami, huku akibainisha kuwa kukamilika kwa sehemu iliyobaki kutategemea upatikanaji wa fedha.
Alisisitiza kuwa mara baada ya kukamilika kwa kipande cha kwanza, serikali itaendelea na ujenzi wa kilomita zilizobaki kadri fedha zitakavyopatikana, kwa lengo la kuhakikisha barabara yote inajengwa kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya usafiri na uchumi wa eneo hilo.
Wananchi wa Iringa na maeneo ya jirani wanaendelea kusubiri kwa matumaini utekelezaji wa ahadi hiyo, wakiamini kuwa barabara hiyo itarahisisha usafirishaji wa bidhaa, hususan chumvi inayozalishwa Pawaga, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda huo.





