Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ally Maulid, ameeleza Tanzania imeendelea kuwa kitovu cha uwekezaji kutokana na kuwepo kwa mazingira rafiki yasiyo na urasimu wala masharti magumu kwa wawekezaji.
Maulid aliyasema hayo Bagamoyo mkoani Pwani wakati akiweka jiwe la msingi la kiwanda cha ROSTAR Tanzania, akimwakilisha Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Alisema hatua ya Serikali kufungua milango ya uwekezaji imekuwa chachu ya kuvutia wawekezaji wengi zaidi, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira nchini.
“Tumefungua milango kwa wawekezaji, mazingira ni rafiki na yanaendelea kuboreshwa ili kukuza sekta ya viwanda na usafirishaji,” alibainisha Maulid.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto za miundombinu ikiwemo barabara na umeme ili kuhakikisha wawekezaji wanafanya kazi katika mazingira bora.
Katika hatua hiyo, aliihakikishia kampuni hiyo kuwa barabara ya kilometa 1.7 kuelekea kiwandani hapo itajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3.4, huku TANESCO ikiwa imekamilisha ujenzi wa njia mbili za umeme wa msongo wa KV 33 kutoka Mlandizi kwa gharama ya sh. bilioni 3.177.
Kwa mujibu Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Bai Xinguo, kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuzalisha magari 5,000 kwa mwaka na tayari kimepokea oda ya magari 1,000.
Alisema uwekezaji wa awamu ya kwanza umegharimu dola za Marekani milioni 20, huku mpango ukiwa kuwekeza zaidi ya dola milioni 60 katika hatua zinazofuata.
Taarifa yake imeeleza kiwanda hicho kimetoa ajira 500, ambapo ajira rasmi ni 300, na kinatarajiwa kupunguza utegemezi wa kuagiza magari kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, alisema mkoa unaendelea kushuhudia ongezeko la viwanda kutoka 1,387 mwaka 2021/2022 hadi 1,722 mwaka 2026.
Naye Mwenyekiti wa CCM Bagamoyo, Abubakar Mlawa, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka sera rafiki za uwekezaji, huku akiomba bidhaa zinazozalishwa mkoani humo ziwe na nembo maalum ya “Made in Bagamoyo/Pwani” ili kutangaza eneo hilo.





