Na John Walter-Babati
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza ujenzi wa daraja linalounganisha Komoto na Sigino, hatua inayotarajiwa kumaliza changamoto ya muda mrefu kwa wananchi wa eneo hilo.
Mwandishi wa Habari hii ameshuhudia mitambo ikiwa kazini ikiendelea na marekebisho ya barabara hiyo, huku vifaa vya ujenzi vikiwa tayari vimewasili eneo la mradi kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi wa daraja hilo.
Daraja hilo linajengwa katika eneo la Legeza, Kijiji cha Gaduwet, Kata ya Sigino wilayani Babati mkoani Manyara, ambako kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakikumbana na adha ya kushindwa kuvuka hasa nyakati za mvua kutokana na korongo kujaa maji.
Hali hiyo imekuwa ikiathiri pia wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi Komoto na shule ya sekondari Komoto, ambao hulazimika kukosa masomo wanaposhindwa kuvuka upande wa pili.
Akizungumzia mradi huo hivi karibuni, Meneja wa TARURA Mkoa wa Manyara, Salim Bwaya, alisema kuwa wana mpango wa kuboresha miundombinu katika maeneo korofi kadri ya upatikanaji wa fedha, akitaja maeneo ya Gallapo na Komoto kuwa miongoni mwa vipaumbele wilayani Babati.
Wananchi wa eneo hilo wameeleza furaha yao, wakisema ujenzi wa daraja hilo ni jibu la kilio chao cha muda mrefu, na wanatarajia litakapokamilika litarahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.





