Na John Bukuku , Dar es Salaam

Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tanzania Industrial Research and Development Organization) limewasilisha teknolojia maalum ya kupima ubora na ufanisi wa majiko katika Kongamano la Kitaifa la Baba Lishe na Mama Lishe lililofanyika Aprili 21, 2026 katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre.

Akizungumza katika kongamano hilo, mtafiti wa teknolojia za nishati kutoka TIRDO, Bw. Gustino Massey, alisema licha ya Tanzania kuwa na utaalamu wa kutengeneza majiko, bado ujuzi huo umetawanyika na haujaunganishwa kuwa mfumo mmoja unaoeleweka na unaoweza kuboresha ubora wa majiko kwa kiwango kikubwa.

Alifafanua kuwa majiko yanayotumika kwa sasa yanatofautiana sana kulingana na malighafi na teknolojia inayotumika kuyatengeneza, hali inayosababisha tofauti kubwa ya ufanisi. Kwa mfano, alieleza kuwa majiko ya mkaa yaliyotengenezwa kwa chuma tupu yana ufanisi mdogo ukilinganisha na yale yenye mchanganyiko wa chuma na udongo wa mfinyanzi, ambayo huhifadhi joto vizuri zaidi.

Kwa mujibu wa Massey, lengo la TIRDO katika kongamano hilo ni kuwaelimisha na kuwahamasisha watoa huduma za chakula maarufu kama Baba Lishe na Mama Lishe kupima majiko wanayotumia ili kubaini kiwango cha ufanisi wake na kufanya maboresho yanayohitajika.

“Tunawakaribisha waje tupime majiko yao kwa kutumia vifaa vya kisasa ili wajue ufanisi wake. Hii itawasaidia kupunguza matumizi ya nishati na gharama za uendeshaji wa shughuli zao,” alisema.

Aliongeza kuwa matumizi ya majiko yasiyo na ufanisi husababisha upotevu mkubwa wa nishati, jambo linaloongeza gharama kwa mpishi na pia kuathiri afya na mazingira kutokana na matumizi makubwa ya kuni au mkaa.

Mbali na ubora wa majiko, TIRDO pia imeelekeza umuhimu wa kubadili tabia za upishi, ikiwemo kuepuka kuwasha jiko bila matumizi ya moja kwa moja, hali inayosababisha upotevu wa nishati na kuongeza gharama zisizo za lazima.

Massey alisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi na majiko yenye ufanisi ni muhimu si tu kwa kupunguza gharama za uendeshaji, bali pia kulinda afya za watumiaji na mazingira kwa ujumla, kwa kupunguza ukataji miti na uzalishaji wa hewa chafu.

Alibainisha kuwa vifaa vilivyoletwa na TIRDO katika kongamano hilo vina uwezo wa kupima kisayansi ubora wa majiko na nishati inayotumika, hatua inayosaidia kutoa tathmini sahihi badala ya kutegemea makadirio ya kawaida.

Kwa ujumla, TIRDO imeeleza kuwa ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali, hususan wajasiriamali wa sekta ya chakula, ili kuboresha teknolojia ya majiko na matumizi ya nishati safi, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kulinda mazingira kwa vizazi vijavyo.