Na Mwandishi Wetu
KIGOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Yusuf Masauni, amefanya ziara katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma, kwa lengo la kujionea hali halisi ya athari za maji na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo kabla ya kuanza kwa mvua za El Niño zinazotarajiwa.
Ziara hiyo imefanyika, Oktoba 17, 2026, ambapo Waziri Masauni ametembelea eneo la Kibirizi na kukagua athari za mafuriko pamoja na uharibifu wa mazingira, kabla ya kuelekea Katubuka, eneo ambalo pia limekumbwa na changamoto ya mafuriko.
Akiwa Katubuka, Mhe. Masauni amewapa pole wananchi walioathirika na mafuriko hayo, huku akiahidi kuwa Serikali itafanyia kazi changamoto zinazowakabili kwa kuzingatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, amewapongeza wananchi kwa kuendelea kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutekeleza wajibu wake wa kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.
Waziri Masauni amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, ikiwemo kutafuta maeneo salama ya kuishi pale inapohitajika, hususan katika kipindi hiki cha maandalizi ya mvua za El Niño. Vilevile, amewahimiza kushirikiana na viongozi wa maeneo yao ili kurahisisha utekelezaji wa hatua zinazochukuliwa na Serikali.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masauni amekagua ujenzi wa mtaro unaolenga kupitisha maji kutoka eneo la Katubuka na kuyaelekeza ziwani, ikiwa ni moja ya hatua zinazolenga kupunguza athari za mafuriko katika eneo hilo.
Waziri Masauni amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuchukua hatua za vitendo katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
“Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan si Serikali ya mchakato na maneno, bali ni Serikali ya vitendo,” amesema Mhe. Masauni, akisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi kwa uzito unaostahili.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kufuatilia changamoto zinazohusiana na mafuriko na uharibifu wa mazingira, pamoja na kuimarisha hatua za tahadhari na utatuzi wa changamoto hizo ili kulinda maisha ya wananchi na mali zao.
Akizungumza kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simoni Sirro, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Dkt. Rashid Chuachua amesema kuanzia mwaka 2023 hadi 2025 Manispaa ya Kigoma Ujiji ilipata mvua zilizokuwa juu ya wastani na kusababisha athari mbalimbali.
“Kata zilizoathirika kwa kiwango kikubwa ni pamoja na Kata ya Katubuka, Kibirizi, Bangwe na Buzebazeba na kupelekea maji kuingia katika nyumba zilizokuwa Jirani na Bwawa la la Katubuka.”
Pamoja na athari hizo kujitokeza Halmashauri ya Manispaa ya Ujiji inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wakazi wa maeneo hayo na maeneo mengine ambayo ni hatarishi.

