Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Songwe lilifanya operesheni maalum ya pamoja ya kukamata wahalifu waliotenda matukio ya kihalifu yakiwepo ya wizi wa magari kuanzia Aprili 10 hadi leo 18, 2026.
Katika operesheni hiyo wamekamatwa watuhumiwa watano pamoja na magari manne yaliyokuwa yameibiwa maeneo mbalimbali Jijini Mbeya.
Waliokamatwa ni pamoja na Lusekelo Stanley Kazimoto maarufu kwa jina la Umeme Mwingi [25] Mkazi wa Kasumulu ambaye amekamatwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T747 DPP. Mtuhumiwa huyu ndiye ambaye uongo unasambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ametekwa.
Watuhumiwa wengine ni Gwakisa Alinanuswe Kulyamo maarufu kwa jina la Gwaki [31] Mkazi wa Kilimahewa Tunduma Mkoa wa Songwe, Deus Nelson Mwamafupa maarufu kwa jina la Super D [38] Mkazi wa Kasumulu Kyela, Michael John Ngonyani [36] Mkazi wa Mtingimbole Mkoa wa Ruvuma na Aizack Simon Luvanda maarufu kwa jina la White [25] Mkazi wa Muungano Tunduma.
Watuhumiwa hawa walikutwa na magari matatu ambayo ni Toyota IST T829 DYP, Toyota Prado T401 DYR na Toyota Spacio T115 DYM. Watuhumiwa kwa uchunguzi wa awali umebaini wamekuwa wakiendesha genge la wizi wa magari nchini na kuyabadilisha namba za usajili na injini namba na kuyapeleka nchi za jirani.
Upelelezi unakamilishwa ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa onyo kwa baadhi ya watu wenye tabia ya kuandaa na kusambaza taarifa za uongo ili kulinda wanaojihusisha na uhalifu kuziacha kwani halitasita kuwakamata. Pia, linatoa onyo kwa mtu au kikundi cha watu wanaojihusisha na uhalifu ikiwemo wizi wa magari kuacha na badala yake watafute kazi nyingine halali za kufanya kwani uhalifu hauna nafasi katika jamii na haulipi.





