Na mwandishi wetu, Mirerani
MACHIMBO ya madini ya Tanzanite, Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, ina migodi 2,000 yenye leseni hai 145 na watu 12,000 wenye kuingia na kutoka kila siku wakiwemo 5,000 wanaolala eneo hilo, haina hospitali wala kituo cha afya, hata zahanati.
Wataalamu watetezi wa haki za binadamu wanaeleza kuwa haki kubwa kuliko zote ni haki ya kuishi kwani ukiwa hai utaweza kupata haki nyingine zilizobaki hivyo ili uishi inapaswa miundombinu ya afya nayo iwepo.
Wataalamu hao wanaeleza kwamba uhai ni muhimu katika maisha ya binadamu ndiyo sababu mtu akiugua au akipata ajali anapelekwa hospitalini, kituo cha afya au zahanati, kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandana hivi karibuni alifanya ziara kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite na kukagua zahanati inayojengwa na kampuni ya Franone Mining waliojitolea kwa ajili ya kutoa matibabu kwa wachimbaji madini.
Kwa ujenzi wa zahanati hiyo katika migodi ya madini ya Tanzanite, kampuni ya Franone Mining chini ya wakurugenzi wake Onesmo Mbise, Francis Matunda na meneja mkuu Vitus Ndakize wanastahili heko.
Zahanati hiyo iliyojengwa na Franone kupitia uwajibikaji kwa jamii (CSR) itakuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji na wadau wote wa madini hasa wenye kipato cha chini na wasio na kipato kwani watanufaika na huduma za afya pindi wakiugua kupitia serikali.
Franone Mining wametumia Sh180 milioni kujenga zahanati hiyo ambayo itakuwa msaada mkubwa kwa wadau wa madini kwani hivi sasa hakuna huduma za afya machimboni pindi mtu akipata tatizo la kiafya zaidi ya huduma za kwanza
Kampuni hiyo imewekeza kwa jamii kwani baada ya kukamilika kwake na kuikabidhi zahanati hiyo kwa serikali, wanufaika wakubwa watakuwa wachimbaji wadogo na wadau wengine wa madini.
Hivi sasa, ili kupata huduma za afya pindi mtu akiugua ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite, inabidi atoke na kufika mji mdogo wa Mirerani ambapo kuna vituo viwili vya afya cha Tanzanite cha kata ya Mirerani na kituo kikongwe cha Mirerani cha kata ya Endiamtu
Zahanati hiyo ya machimboni ikikamilika na kuanza kutoa huduma, wachimbaji watanufaika kwa kupimwa magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria, homa ya matumbo, kifua, kupata matibabu, kulazwa pindi wakiugua na ushauri nasihi wa kiafya.
Kitendo cha kujengwa zahanati hiyo ndani ya ukuta ni suala la kupongezwa kwa aliyebuni wazo kwani ni manufaa makubwa mno kwa wachimbaji ambao awali walikuwa wanapata changamoto ya kutibiwa pindi wakihitaji huduma hiyo.
Zahanati hiyo pindi ikikamilika itatoa nafasi pia kwa wataalamu wa magonjwa ya kupumua kutoka hospitali ya kifua kikuu ya Kibong’oto kutoka wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, kuwa na kiliniki ya magonjwa ya kifua kikuu na mapafu kwa lengo la kuwapima na kutoa matibabu.
Zahanati hiyo itakuwa ni manufaa makubwa kwa wadau wa madini ya Tanzanite kwani hata wataalamu wa afya watakuwa karibu kwa kutoa elimu ya uchimbaji hasa kuepuka vumbi katika uchimbaji wao ili wasipate maradhi ya kifua na mapafu.
Tumeona na kusikia baadhi ya wagonjwa wakiwa Kibong’oto wakilalamika kupata maradhi ya vifua na mapafu kutokana na kutokuwa na elimu ya kuepuka vumbi pindi wakichimba.
Zahanati hiyo ikikamilika tunatarajia elimu itakuwa inatolewa na uchimbaji wa salama wa kuepuka vumbi kwa kumwaga maji ya kutosha mgodini itafanyika kwa lengo la kuepuka maradhi ya kifua na mapafu.
Franone Mining chini ya wakurugenzi wake Onesmo Mbise, Francis Matunda na meneja mkuu Vitus Ndakize, siyo tuu wanajenga zahanati hiyo, pia wamekuwa wakisaidia jamii kwenye shule za msingi na sekondari, kukarabati barabara, ujenzi wa njia ya kupita eneo la kuhifadhi miili kwenye kituo cha afya Mirerani na wanaoathirika na mafuriko yakitokea tarafa ya Moipo.
Kutokana na hali hiyo, jamii inayowazunguka wawekezaji hao wanapaswa kuwaunga mkono katika shughuli zao za uchimbaji wa madini na siyo kuingia nao migogoro isiyo na tija ambayo itasababisha ukwamishaji wa shughuli zao.
Pia, wachimbaji wengine wa madini ya Tanzanite muige mfano wa kampuni ya Franone Mining katika kusaidia jamii inayowazunguka, siyo vyema mnapata madini katika eneo hilo na kuondoka bila kuacha alama katika upande wa sekta ya elimu au afya.




