Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
JUMLA ya miradi 68 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 263.1 mkoani Pwani inatarajiwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru katika wilaya saba zenye halmashauri tisa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, alisema hayo Aprili 18, 2026 wakati akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka mkoa wa Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Mtambani, Mapinga wilayani Bagamoyo.
Alisema kati ya miradi hiyo, miradi 23 itawekewa mawe ya msingi, 17 itazinduliwa na 24 itakaguliwa.
Baada ya makabidhiano ya kimkoa, Kunenge alimkabidhi Mwenge huo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, ambaye alisema wilaya hiyo ina halmashauri mbili, Bagamoyo na Chalinze ambapo katika Halmashauri ya Bagamoyo, miradi minane yenye thamani ya sh bilioni 11.4 imepitiwa.
Katika miradi hiyo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameweka jiwe la msingi katika mradi wa kusogeza huduma ya maji safi wa Kibosha–Mapinga unaosimamiwa na DAWASA, utakaogharimu sh milioni 182.6, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 80.
Alieleza chanzo cha maji cha mradi huo ni tanki la Vikawe lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni sita, na unatarajiwa kuhudumia kaya 500, huku kaya 15 tayari zikiwa zimeunganishwa na zoezi la kuunganisha wateja likiendelea.
Mradi huo unalenga kuhudumia wakazi 11,084 wa Kitongoji cha Kibosha, ambapo kwa sasa watu 2,919 wanapata huduma ya maji.
Mwang’onda alisema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi.





