Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy akizungumza kwenye kikao cha kijadili mpango kazi na bajeti ya mwaka 2026/2027 kilifanyika Jijini Mwanza
Mkuu wa Mkoa Said Mtanda akizungumza kwenye mkutano WA kwanza uliowakutanisha REA na Wadau wa maendeleo
Washiriki wa kikao wakiwa ukumbini
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wameeleza vipaumbele vitano vilivyopo kwenye mpango kazi wao katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Hayo yamesemwa leo Aprili 17, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy katika mkutano wa kwanza wa mwaka uliowakutanisha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wadau wa Maendelo Jijini Mwanza.
Amesema lengo la kukutana kwenye kikao hicho ni kujadili mpango kazi na bajeti ya mwaka ujao wa fedha sanjari na kuwaonesha wadau wa maendeleo fedha wanazozitoa kwenye miradi ya Nishati Vijijini zinavyotumika
Akieleza vipaumbele hivyo Mhandisi Saidy amesema ni kuharakisha upelekaji wa umeme katika vitongoji elfu 14 vilivyobakia,mpango maalumu wa kuwezesha na kuharakisha uunganishaji umeme majumbani kwa wananchi,kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia katika maeneo ya vijijini,kuwezesha miradi ya nishati jadidifu pamoja na kuongeza ufanisi katika matumizi ya umeme na utumiaji wa umeme kwa shughuli za maendeleo.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Bodi REA, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amesema bajeti ya Wakala wa Nishati Vijijini inategemea fedha kutoka Serikalini na kwa wadau wa maendeleo ambao ni World Bank,Serikali ya Norway,Serikali ya Sweden, UNDP pamoja na Wakala wa Maendeleo Ufaransa (AFD)
Awali akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema miradi ya umeme inayotekelezwa mkoani humo ni pamoja na kupeleka umeme kwenye vitongoji,mradi wa usambazaji wa majiko banifu kwa bei nafuu,mradi wa ufungaji wa mifumo ya umeme jua majumbani,mradi wa kuvua na kukausha dagaa kwakutumia nishati ya umeme jua pamoja na mradi wa usambazaji wa nishati safi ya kupikia kwa jeshi la magereza.
Aidha, amesema wataendelea kushirikiana katika kuhakikisha wanaiangalia na kuilinda miradi yote inayotekelezwa na REA huku akiongeza kuwa hawatasita kuchukua hatua Kwa wale ambao wanania ya kukwamisha miradi hiyo.
Mtanda amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutunza mazingira hasa katika matumizi makubwa ya kuni na mkaa kwani yanaendelea kusababisha uharibifu wa mazingira.





