Na WMJWM-Morogoro.
Kamati ya Kitaifa ya Kushughulikia Malalamiko ya Mradi wa Kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili wa kijinsia (PAMOJA), imeshauriwa kutumia lugha rahisi katika kupitia na kufanya maboresho ya rasimu ya muongozo utakaotumika katika kushughulikia malalamiko wakati wa utekelezaji wa mradi huo ili kuwawezesha wanufaika kuelewa kwa urahisi taratibu wanazotakiwa kuzifuata katika kuwasilisha malalamiko yao.
Ushauri huo umetoleo mkoani Morogoro na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felista Mdemu wakati anafungua kikao kazi cha Kamati hiyo chenye lengo la kuwajengea uwezo wajumbe na kuboresha rasimu ya mwongozo iliopo ili iweze kuendana na mahitaji halisi ya utekelezaji wa mradi pamoja na kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa, ikiwemo miongozo ya Benki ya Dunia.
Mdemu amesema muongozo ni nyenzo muhimu katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau. Kupitia mfumo wa upokeaji wa maoni na malalamiko kutoka kwa jamii, kushughulikia changamoto kwa wakati, kujifunza na kuboresha utekelezaji mzima wa shughuli za mradi.
“Imani yangu ninyi wataalamu mliopo hapa ni wabobezi katika kushughulikia malalamiko na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati. Hivyo nitoe rai kwenu kutumia ujuzi wenu kuboresha mwongozo huu ili uendane na uhalisia wa mazingira katika Mikoa na Halmashauri zetu”. amesema Mdemu.
Aidha, amewasihi kujadili kwa kina kwa uwazi na kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha tunapata mwongozo ulio bora, unaotekelezeka na unaozingatia mahitaji ya makundi yote, hususan wanawake ambao ndio walengwa wakuu wa mradi huu wa PAMOJA.
Naye Mratibu wa Mradi wa PAMOJA, Adventina Kato amesema mradi huo umelenga kupunguza kwa kiwango kikubwa na hatimaye kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, ambavyo vimekuwa tishio katika jamii huku akibainisha kuwa kuwawezesha wanawake kiuchumi ni njia mojawapo ya kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kujilinda dhidi ya mazingira hatarishi.
Kwa upande wake, Afisa Sheria Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Happy Msimbe amesema mwongozo huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya ikiwa ni pamoja na kupunguza malalamiko, kuimarisha usimamizi wa haki na kuongeza imani ya wananchi katika utekelezaji wa mradi huo.
Kwa Upande wake Josephine Zimba Mwezeshaji Mwakilishi wa Benki ya Dunia alitoa ufafanuzi juu ya sifa na vigezo muhimu ya miongozo ya miradi inayofadhiliwa au kukopeshwa na benki ya dunia ambayo pia miongozo hiyo itawasadia katika kuendesha mradi huu wa PAMOJA.
Mradi wa PAMOJA unatarajiwa kuwa suluhisho endelevu katika kupambana na ukatili wa kijinsia huku ukichangia maendeleo jumuishi kwa wanawake na jamii kwa ujumla.





