Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imebainlnisha kuwa imejipanga kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo pamoja na kuimarisha mikakati ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika mnyororo wa thamani ya mazao ya kipaumbele.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameyabainisha hayo Aprili 17, 2026 bungeni Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, huku Ofisi ya Rais Ikulu imeomba kuidhinishiwa shilingi bilioni 39,416,152,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Aidha amebainisha kuwa Ofisi ya Rais na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri zimeomba kuidhinishiwa shilingi trilioni 1,382,937,944,000, ambapo kati ya fedha hizo shilingi trilioni 1,256,299,943,000 sawa na asilimia 90.84 ni kwa matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 125,408,015,000 sawa na asilimia 9.07 ni kwa miradi ya maendeleo kwa fedha za ndani, na shilingi bilioni 1,229,999,000 sawa na asilimia 0.09 ni kwa miradi ya maendeleo kwa fedha za nje.
Pia ameongeza kuwa kwa upande wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imepanga kupokea na kuhakiki matamko ya rasilimali na madeni ya viongozi wa umma pamoja na kuchunguza tuhuma za uvunjifu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Aidha amebainisha kuwa katika mwaka huo wa fedha, Sekretarieti hiyo imeomba kuidhinishiwa shilingi bilioni 18,074,774,000, ambapo shilingi bilioni 15,074,774,000 sawa na asilimia 83.40 ni kwa matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 3 sawa na asilimia 16.60 ni kwa miradi ya maendeleo.
Pia ameongeza kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imepanga kushughulikia vibali vya ajira mpya 45,000, kuhakiki na kuidhinisha madai ya malimbikizo ya mishahara katika taasisi 425 pamoja na kufanya uhakiki wa watumishi katika taasisi 127.
Aidha amebainisha kuwa majukumu mengine ni pamoja na kutoa vibali vya ajira mbadala kwa watumishi 7,124, kuidhinisha madai ya malimbikizo ya mishahara kwa waajiri 206 pamoja na kutekeleza Programu ya Maboresho ya Mfumo wa Utumishi wa Umma inayogharamiwa kwa fedha za ndani na nje kupitia Benki ya Dunia.
Pia ameongeza kuwa katika kuboresha huduma za utumishi, Serikali itaendelea kutoa huduma kwa viongozi wa kitaifa wastaafu 21 kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia Chuo cha Utumishi wa Umma (TPC), amesema kuwa chuo hicho kimepanga kuendeleza programu mpya 15 za mafunzo katika uongozi, usimamizi na utawala, kutoa mafunzo kwa watumishi 10,000 pamoja na kufanya tafiti tumizi 14 na machapisho 20.
Aidha amebainisha kuwa taasisi ya Watumishi Housing Investment imepanga kukamilisha ujenzi wa nyumba 74 za watumishi wa afya na elimu, kuanza ujenzi wa nyumba 132 mpya wilayani, pamoja na kukamilisha nyumba 66 na kuanza ujenzi wa nyumba 82 katika mradi wa ghorofa wa Kisasa Hilltop Njedengwa jijini Dodoma.
Pia ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeomba kuidhinishiwa shilingi bilioni 84,888,399,000, ambapo shilingi bilioni 55,832,858,000 sawa na asilimia 65.77 ni kwa matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 29,055,541,000 sawa na asilimia 34.23 ni kwa miradi ya maendeleo.




