Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeiomba Bunge kuidhinisha jumla ya takribani shilingi trilioni 1.5 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni Aprili 17,2026 Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema fedha hizo zitawezesha kuimarisha utendaji wa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais, kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na kuendeleza maboresho ya mfumo wa utumishi wa umma nchini.
Akizungumza juu ya bajeti hiyo amesema kuwa inahusisha matumizi ya taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri na taasisi nyingine zilizo chini ya ofisi hiyo, ambapo sehemu kubwa ya fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku sehemu nyingine ikienda kwenye miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za umma na miundombinu ya utawala.
Aidha, katika hotuba yake, Mhe. Kikwete imeeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha utumishi wa umma, ikiwemo kushughulikia vibali vya ajira zaidi ya nafasi 45,000 za ajira mpya, kuhakiki malimbikizo ya mishahara katika taasisi zaidi ya 425 pamoja na kufanya uhakiki wa watumishi katika taasisi 127 ili kuboresha usahihi wa taarifa za kiutumishi na mishahara.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imepanga kuimarisha Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuendelea kupokea na kuhakiki matamko ya mali na madeni ya viongozi, pamoja na kuchunguza tuhuma za uvunjifu wa maadili kwa mujibu wa sheria, hatua inayolenga kuongeza uwazi na uwajibikaji katika uongozi wa umma.




