Na Silivia Amandius.
Bukoba.
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekutana na wadau wa usafiri wa majini mkoani Kagera kukusanya maoni kuhusu athari za mabadiliko ya bei ya mafuta na uwezekano wa kurekebisha nauli za abiria, katika jitihada za kuhakikisha kunakuwa na uwiano unaolinda maslahi ya wananchi na watoa huduma.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji, Issaya Tendega, amesema Serikali itahakikisha maoni yote yanayokusanywa yanawasilishwa katika mamlaka husika na kufanyiwa kazi kwa wakati, huku akisisitiza kuwa majibu yatarejeshwa kwa wadau kabla ya Aprili 26, 2026 ili kuwezesha maamuzi sahihi.
Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa ELCT Manispaa ya Bukoba April 16, mwaka huu uliwakutanisha wafanyabiashara, wasafiri na wamiliki wa vyombo vya majini, ambapo walijadili kwa kina athari za kupanda kwa bei elekezi ya mafuta iliyoanza kutumika Aprili Mosi mwaka huu na namna inavyoathiri gharama za uendeshaji wa huduma za usafiri majini.
Afisa Uhusiano wa TASAC Kanda ya Ziwa, Said Mkabakuli, amesema lengo la shirika hilo ni kulinda maslahi ya wananchi pamoja na watoa huduma kwa kuhakikisha kunakuwa na uwiano katika mabadiliko ya nauli, ili wananchi waweze kuendana na gharama bila kubebeshwa mzigo mkubwa, huku huduma bora zikiendelea kutolewa. Ameongeza kuwa TASAC inaendelea kupokea maoni ya wadau kwa njia ya mdomo na maandishi ili kupata uamuzi jumuishi.
Kwa upande wa wadau, baadhi yao akiwemo Mwalimu Ivona Bajumuzi, wameipongeza TASAC kwa kuwashirikisha wananchi katika mchakato huo, wakieleza kuwa hatua hiyo inasaidia kuongeza uelewa pale ambapo mabadiliko ya nauli yanapotokea. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameeleza hofu juu ya ongezeko la nauli, wakitaka kuwepo kwa suluhisho litakalopunguza gharama bila kuathiri maisha ya watumiaji wa huduma hiyo.





