Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, akizungumza wakati wa Mkutano wa Wadau wa Tasnia ya Pamba uliofanyika Aprili 16, 2026 jijini Dodoma
Washiriki wa Mkutano wa Wadau wa Tasnia ya Pamba wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa mkutano huo uliofanyika Aprili 16, 2026 jijini Dodoma.
Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha sekta ya kilimo kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao, hususan zao la pamba.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema mifumo ya upatikanaji wa pembejeo imeboreshwa ili kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati na kwa gharama nafuu, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha wakulima.
Amesema juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza mchango wa zao la pamba katika uchumi wa taifa pamoja na kukuza uchumi wa wakulima na nchi kwa ujumla.
Ameyasema hayo Aprili 16, 2026 jijini Dodoma wakati wa Mkutano wa Wadau wa Tasnia ya Pamba, ambapo alisisitiza kuwa uboreshaji wa huduma za ugani unapaswa kwenda sambamba na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kuimarisha sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia na zana bora za uzalishaji.
Hata hivyo, amesema bado wakulima wengi wanatumia mbinu za kizamani za kilimo, hali inayochangia kushuka kwa tija hata kwa wale wenye mashamba makubwa.
Kutokana na changamoto hiyo, Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuwahamasisha wakulima kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emanuel Cherehani, ameishauri Serikali kuunda mfumo madhubuti wa kusimamia vyama vya ushirika ili kuongeza tija kwa wakulima wa pamba nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania, Bw. Marco Mtunga, amesema bado kuna changamoto katika ugawaji wa pembejeo, matumizi ya mizani pamoja na usimamizi wa ubora wa pamba wakati wa mauzo, hali inayochangiwa na ukosefu wa mamlaka ya kutosha kwa wasimamizi wa vyama vya ushirika kuwachukulia hatua wanaokiuka taratibu.





