Na Maelezo Zanzibar 01.04.2026
Waziri wa Maji, Nishati na Madini Mhe Nadir Abdullatif Al-wardy amesema viongozi wanaendelea kujifunza nidhamu, uadilifu na kuwatumikia wananchi kwa kufata misingi ya haki na uwajibikaji kutoka kwa waasisi wa taifa waliotangulia.
Mhe. Nadir ameseyasema hayo katika ziara ya kumuombea dua katika kaburi la aliyekuwa Luteni Kanali Mstaafu, Marehemu Said Iddi Bavuai huko Shakani Wilaya ya Magharibi B.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuwaenzi na kuthamini jitihada walizozitoa waasisi waliopita katika kupigania taifa.
Aidha amefahamisha kuwa licha ya viongozi hao kutangulia mbele ya haki lakini Serikali bado inaendelea kujifunza mambo mengi ya kiutendaji kutoka kwao.
Ameeleza kuwa Serikali inaungana na familia ya Marehemu huyo kwa kumuombea dua kwani walioyafanya katika nchi ni makubwa na kupigiwa mfano na akatumia fursa hiyo kuipongeza serikali kwa kuweka utaratibu wa kufanya dua kwa viongozi hayo kwani inaongeza mapenzi huruma na uadilifu.
Kwa upande wao Wanafamilia hiyo wameishukuru Serikali kwa kuandaa dua kwa ajili ya wasisi waliotangulia na kuomba dua hizo kuwa endelevu kwani viongozi hao wanamchango mkubwa katika kuleta amani na utulivu katika nchi.





