Mafundi wa kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation(CCECC) wakiendelea na kazi ya ujenzi wa tenki la maji katika kijiji cha Mahilo Manispaa ya Songea ambalo ni sehemu ya mradi wa maji wa Miji 28 unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 115.77.
Mhandisi wa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea Vicent Bahimana aliyeshika fimbo,akimuonyesha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi Taifa Fadhil Manganya mchoro wa mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa na Serikali kupitia Souwasa kwa gharama ya Sh.bilioni 145.77 ambao hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 6.5,katikati Mkurugenzi Mtendaji wa Souwasa Mhandisi Patrick Kibasa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi Taifa Fadhil Manganya,akikagua ujenzi wa tenki la maji linalojengwa katika kijiji cha Mahilo Manispaa ya Songea ikiwa ni sehemu ya mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa katika Manispaa ya Songea kwa gharama ya Sh.bilioni 145.77,kushoto Mkuu wa wilaya ya Songea Kapenjama Ndile.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma(Souwasa)Mhandisi Patrick Kibasa,akimueleza Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya Chama cha Mapinduzi Taifa Fadhil Manganya hatua ya mradi wa maji wa miji 28 unavyoendelea,kulia Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma Mohamed Khalfan.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi Taifa Fadhil Manganya,akizungumza na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mahilo kata ya Ndilimalitembo baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa na Serikali katika Manispaa ya Songea kwa gharama ya Sh.bilioni 145.77.
…………
Na Mwandishi Wetu, Songea
Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa)imesema,mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa katika Manispaa hiyo kwa gharama ya Sh.bilioni 145.77 ndiyo suluhisho la changangomoto ya upungufu wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa Manispaa ya Songea.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Souwasa Mhandisi Patrick Kibasa amesema hayo jana,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama cha Mapinduzi Fadhil Maganya.
Kibasa alisema,mradi huo ni jibu na suluhisho la kudumu kwani utaongeza upatikanaji wa majisafi,kuboresha miundombinu ya maji na kuhakikisha huduma bora ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Songea.
Kibasa alisema,mkataba wa utekelezaji wa mradi huo ulisainiwa tarehe 10 Machi 2023 kati ya wizara ya maji na mkandarasi kampuni ya China Civil Engineering Contruction Corporatino(CCECC) na mkandarasi ameanza utekelezaji tangu tarehe 2 Januari 2024 na hadi sasa umefikia asilimia 6.5.
Kwa mujibu wa Kibasa,mradi huo unahusisha ujenzi wa kidaka maji(Intake)katika mto Njuga uliopo kijiji cha Kikunja Halmashauri ya wilaya Songea chenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 17.0 kwa siku.
Alitaja kazi nyingine zinazotekelezwa ni kujenga mtambo wa kisasa wa kuchuja maji,kusafisha na kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 16 kwa siku ili kuhakikisha ubora wa maji kwa matumizi ya binadamu,ujenzi wa matenki matatu yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita milioni 9 za maji.
“katika mradi huu mkubwa tutalaza bomba za kusafirisha maji zenye urefu wa kilometa 30.2 kutoka kwenye chanzo mpaka kwenye matenki,kulaza bomba za kusambaza maji zenye urefu wa kilometa 34,kukarabati miundombinu ya mtambo wa kuchuja maji na kusafisha maji uliopo eneo la Matogoro wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 11.5 kwa siku”alisema Kibasa.
Ametaja kazi zilizofanyika ni usanifu wa miundombinu ya njia ya bomba za kusafirisha maji,kidaka maji,mtambo wa kuchuja na kusafisha maji,ujenzi wa matenki mawili yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 1 kila moja katika maeneo ya maji Wilaya na Chandamali na ujenzi wa tenki la lita milioni 5 katika eneo la Mahilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 70.
Kibasa,ametaja faida za mradi huo utakapokamilika ni kuongezeka kwa watu watakaopata majisafi na salama kutoka asilimia 96 mpaka kufikia asilimia 100 na ubora wa maji utaimarika kutokana na ujenzi wa miundombinu ya kisasa na ukarabati wa mitambo ya kuchuja maji.
Alisema,mradi huo utakuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira kwani pamoja na changamoto zilizopo,ushirikiano kati ya serikali,wakazi na wadau wengine unahitaji ili kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu na kuleta manufaa ya muda mrefu kwa jamii.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Taifa ya Chama cha Mapinduzi Fadhil Maganya,amemtaka mkandarasi kukamilisha kazi kwa wakati na kwa ubora licha ya kuwepo kwa changamoto kwani wananchi wa Manispaa ya Songea wanahitaji sana maji.
“Naiomba Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ilete fedha ili kukamilisha mradi huu ambao utakuwa mkombozi mkubwa,wananchi wana hamu kubwa ya kupata huduma ya majisafi na ya uhakika kwenye maeneo yao”alisema Maganya.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Mohamed Khalfan amewapongeza wataalam wa Souwasa kwa kusimamia vema mradi huo ambao ukikamilika utakuwa suluhisho la kudumu la upungufu wa maji kwa wakazi wa manispaa ya Songea na maeneo mengine ya jirani.




