DENIS MLOWE, DAR ES SALAAM
KOCHA wa Tanzania Prison Volleyball Club, Dismas Dick Amiri, amesema timu yao inaendelea vizuri na maandalizi ya kushiriki Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya timu hiyo, Amiri alisema kuwa wapo katika wiki ya tatu ya maandalizi baada ya timu kuwa mapumzikoni kwa muda mrefu alieleza kuwa katika kipindi hiki wamezingatia kufuata taratibu zote muhimu za maandalizi ili kuhakikisha timu inakuwa katika kiwango kizuri kabla ya kuanza kwa mashindano.
Alisema mazoezi ya awali yalijikita zaidi katika kujenga utimamu wa mwili kwa wachezaji, ambapo walifanya mazoezi ya uvumilivu, kasi, nguvu pamoja na wepesi. Baada ya kukamilisha hatua hiyo, sasa timu imeanza kufanya mazoezi ya kucheza mpira ili kuboresha udhibiti wa mpira pamoja na mbinu na ufundi wa mchezo.
Kwa mujibu wa kocha huyo, mazoezi yanafanyika katika Chuo cha Kampala kilichopo Gongolamboto kila siku za Jumamosi na Jumapili kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni.
Amiri alisema kwa sasa hali ya timu ni nzuri kwani hata baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi au wagonjwa wamesharejea na wako katika hali nzuri kiafya.
Ameongeza kuwa wachezaji wana morali kubwa na wanajipanga kuhakikisha wanashinda ubingwa wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Alifafanua kuwa ushindi wa ubingwa wa mkoa unaweza kuipa timu nafasi ya kushiriki Ligi ya Taifa ya Volleyball nchini Tanzania, jambo ambalo ni moja ya malengo makubwa ya timu hiyo katika msimu huu.
Kocha Amiri pia aliwahakikishia mashabiki na wadau wa Tanzania Prisons kuwa timu iko katika hali nzuri na inaendelea kufanya maandalizi kwa umakini ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Aidha, aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenda kuishangilia timu yao katika mechi zitakazochezwa katika Chuo cha Kampala, Gongolamboto.
Katika ratiba ya mechi za mwishoni mwa wiki hii, siku ya Jumamosi kutakuwa na mchezo wa wanaume kati ya Tanzania Prisons Volleyball dhidi ya Air Force, timu ya Jeshi la Anga. Mchezo huo utachezwa katika uwanja wa Chuo cha Kampala kuanzia saa tano asubuhi.
Siku ya Jumapili kutakuwa na mchezo wa wanawake kati ya Tanzania Prisons Volleyball dhidi ya Chui ya Lugalo, timu kutoka Jeshi la Lugalo. Michezo yote itachezwa katika uwanja huo wa Chuo cha Kampala uliopo Gongolamboto.
Kocha Amiri alitumia pia nafasi hiyo kutoa shukrani zake za pekee kwa Mkuu wa Jeshi la Magereza, Afande Katungu, kwa kutoa fursa na mazingira mazuri ya timu kushiriki katika mashindano hayo pamoja na kupata muda wa kufanya maandalizi.
Pia alimshukuru Mkuu wa Chuo cha Taaluma na Urekebishaji Tanzania (TCTA), Afande Kaomuza, kwa kuwapa ushirikiano na baraka zote zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa kwa maandalizi yanayoendelea, wana imani kubwa ya kufanya vizuri katika mashindano hayo na kuiwakilisha vyema Tanzania Prisons.
