Msimu wa tatu wa Bunge Marathon umezinduliwa leo jijini Dar es Salaam ambapo mwaka huu mbio hizo zinatarajiwa kufanyika tarehe 18 Aprili 2026 Jijini Dodoma.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti wa Maadalizi ya mbio hizo Mhe. Festo Sanga amesema mbio hizo ambazo zinaandaliwa kwa mara tatu, zinatarajiwa kuwakutanisha wanariadha zaidi ya 5,000 kutoka ndani nan je ya Tanzania. 

Amesema Lengo la kuendeleza mbio hizi ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuimarisha afya kupitia michezo.

“Mbio hizi zitawakutanisha Watunga Sheria na wananchi wao pamoja na wanariadha wengine zaidi ya 5,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania, ambapo pamoja na kuimarisha afya watashiriki kuchangia maendeleo ya nchi yao” alisema Mhe. Sanga

Mheshimiwa Sanga amesema mbio hizo zitakuwa za nusu marathon yaani kilomita 21, kilomita 10 na kilomita 5 na zinakuwa ni tukio muhimu kwa wapenda michezo na wafuasi wa maendeleo.

Mhe. Sanga amesema dirisha la usajili wa mbio hizi limefunguliwa rasmi kupitia tovuti ya maalum ya Bunge Marathon www.marathon.bunge.go.tz ambapo ada ya ushiriki wa mbio hizo ni shilingi elfu arobaini (40,000/-) ambayo mshiriki atapatiwa Marathon Kit itakayojumuisha fulana, mfuko na namba ya kukimbilia.

Akizungumzia zawadi za washindi Mheshimiwa Sanga amesema zawadi katika msimu huu wa tatu zimeboreshwa zaidi ambapo kwenye nusu marathon yaani kilometa 21, mshindi wa kwanza atajinyakulia Milioni 6, mshindi wa pili atapata Milioni 3 na mshindi wa tatu akiambulia Milioni 1.5.

Kwa upande wa kilomita 10, mshindi wa kwanza atazawadiwa shilingi milioni 3, mshindi wa pili Shilingi milioni 2, na mshindi wa tatu atajinyakulia shilingi milioni moja, huku katika kilomita 5 mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 2, nafasi ya pili akipata milioni moja na mshindi wa tatu atapata shilingi laki tano.

Kuhusu mgeni rasmi Mheshimiwa Sanga amesema atatangazwa hivi karibuni na kuwahakikishia kuwa kutakuwa na matukio maalum ya kushtukiza kwa washiriki wenye ulemavu, kuhakikisha ushirikishwaji katika mbio hizo.

 

Katika hatua nyingine Mh Sanga amesema mbali na mambo mengine kupitia mbio hizo Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azzan Zungu Spika ameelekeza mbio hizo kutumika kuchangia damu salama ikiwa ni lengo la kuwaunga mkono watu wa damu salama lakini pia kuonesha umoja wao kwa wananchi.Kwa upande wake Mkurugenzi wa Silent Ocean Ndg Mohamed Soloka amesema Bunge Marathon imebeba agenda zao zote ambazo ni afya na michezo, ndio maana wakashawishika kudhamini mbio hizo.

“Tumevutiwa na lengo la mbio hizi ndio maana tumedhamini, tunaunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kutumia michezo kuimarisha afya za Watanzania, lakini pia kama ajira kwa maendeleo mapana ya taifa letu “ amesema Soloka

Aliongeza kuwa “Niwaahidi wanariadha na wapenda michezo wote nchini, Bunge Marathon msimu wa tatu, itakuwa kubwa na bora zaidi, niwaombe mjitokeze kwa wingi kujisajili na kushiriki mbio hizi” 

Amesema katika udhamini huo Kampuni ya Silent Ocean ambao ndio wadhamini wakuu wa mbio hizo watatoa medali, traksuti, tshirt na vifaa vyote vya Bunge Marathon.