NA DENIS MLOWE, IRINGA
IDARA ya Vijana ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa kupitia Usharika wa Kanisa Kuu Iringa, kwa kushirikiana na huduma ya The Healing Missionaries, imeandaa mkesha mkubwa wa kusifu utakaofanyika Machi 20 mwaka huu mkoani Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, KheriJames, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kuongoza tukio hilo la kiroho linalolenga kuwakutanisha waumini na wananchi kwa pamoja katika kumsifu na kumshukuru Mungu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Luckson Luswema maarufu kama Kaka Mtumishi, amesema mkesha huo umeandaliwa kwa lengo la kumrudishia Mungu utukufu kwa mambo makuu aliyowatendea waumini, huku akiwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki ibada hiyo ya baraka.
Amesema kuwa mgeni mwenyeji atakuwa Askofu wa Dayosisi ya Iringa, Askofu Blaston Gaville, ambaye ataungana na viongozi mbalimbali wa dini katika kuongoza ibada hiyo maalum.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa The Healing Missionaries, Patrick Mulunda, amesema taasisi hiyo imejikita katika kueneza Injili hasa katika maeneo ambayo huduma za kiroho bado hazijafika ili kuwafikia watu wengi zaidi.
Mkesha huo pia unatarajiwa kupambwa na waimbaji mbalimbali wa nyimbo za injili, viongozi wa dini na viongozi wa kijamii, na hivyo kuufanya kuwa tukio la kipekee kwa wakazi wa Iringa na maeneo ya jirani.

