Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Kikao cha Umoja wa Afrika (AU) kuhusu masuala ya G20, katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 14 Februari, 2026.
Rais Dkt. Samia aliwasilisha msimamo wa Tanzania kuhusu vipaumbele vya maendeleo, ikiwemo kuimarisha matumizi ya nishati safi, usimamizi wa madeni ya nchi, ustahimilivu dhidi ya majanga ya tabianchi, uongezaji thamani wa rasilimali za madini, pamoja na kuimarisha usalama wa chakula.
………..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameshiriki kikao cha Umoja wa Afrika (AU) kilichojadili taarifa ya matokeo ya Mkutano wa Viongozi wa G20 uliofanyika Novemba 22 hadi 23, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, kikao hicho kilipokea na kujadili taarifa iliyowasilishwa na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ambaye aliandaa na kuongoza mkutano wa kwanza wa G20 kufanyika barani Afrika.
Akinukuliwa katika taarifa hiyo, Rais Dkt. Samia alimpongeza Rais Ramaphosa kwa mafanikio hayo, akieleza kuwa ni hatua ya kihistoria kwa bara la Afrika.
“Hatua hii ya kihistoria ni fahari kwa Afrika na ni uthibitisho wa kuongezeka kwa ushawishi wa bara letu katika kuunda mijadala ya kimataifa na kutafuta suluhisho za changamoto zinazoikabili dunia,” alinukuliwa Rais Samia.
Akizungumzia vipaumbele vilivyobainishwa katika Azimio la G20, Rais Dkt. Samia alisisitiza masuala muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, yakiwemo kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga, usimamizi madhubuti wa madeni ya nchi, kuongeza matumizi ya nishati safi, kuongeza thamani ya madini, pamoja na kuimarisha usalama wa chakula.
Kuhusu majanga, Rais Samia aliipongeza G20 kwa dhamira ya kuongeza juhudi za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, akibainisha kuwa Afrika inaendelea kuathirika zaidi na majanga ya asili.
Katika eneo la uhimilivu wa madeni, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa madeni ili kuwezesha nchi za Afrika kuwekeza zaidi katika miundombinu, sekta ya afya na ulinzi wa kijamii.
Aidha, Rais Samia alieleza kuunga mkono dhamira ya G20 ya kuongeza matumizi ya nishati safi, akisisitiza kuwa nishati ya uhakika ni msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii, huku akithibitisha kuendelea kutekeleza jukumu lake kama Bingwa wa Nishati Safi ya Kupikia barani Afrika.
Akizungumzia sekta ya madini, Rais Samia alisema kupitishwa kwa Mfumo wa G20 wa Madini Muhimu kunatoa fursa kwa Afrika kuchakata na kuongeza thamani ya rasilimali zake badala ya kuuza malighafi pekee. Alitaja madini muhimu yaliyopo Tanzania kuwa ni pamoja na nikeli, grafiti na lithiamu, yanayotumika katika teknolojia za kisasa na nishati safi.
Kuhusu usalama wa chakula, alisisitiza haja ya kuimarisha uzalishaji wa kilimo na kuwasaidia wakulima wadogo ili kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa chakula.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu Tanzania, Rais Samia pia amepongeza kupatikana kwa uanachama kamili wa Afrika ndani ya G20 pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa ushirikiano wa kifedha barani humo, akisema hatua hizo zinaimarisha nafasi ya Afrika katika uchumi wa dunia.
Kikao hicho kilihitimisha kwa kusisitiza kuongezeka kwa sauti ya Afrika katika majukwaa ya kimataifa na dhamira ya bara kushiriki kikamilifu katika kutafuta suluhisho za changamoto za pamoja za dunia.
