Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Namibia Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Ziara ya Kitaifa, tarehe 20 Juni, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Namibia Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 20 Juni, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo rasmi na Ujumbe wa Namibia uliongozwa na Rais wa nchi hiyo Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 20 Juni, 2026.
…………
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema uhusiano kati ya Tanzania na Namibia una msingi wa kihistoria uliojengwa wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, na sasa mataifa hayo mawili yamedhamiria kugeuza urafiki huo kuwa ushirikiano wenye tija katika maendeleo ya kiuchumi.
Amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, aliyefanya ziara yake ya kwanza rasmi ya Kitaifa nchini Tanzania tangu alipochaguliwa kuwa Rais wa Namibia, akieleza kuwa ziara hiyo ni ishara ya kuendelea kuimarishwa kwa uhusiano wa karibu kati ya nchi hizo.
Rais Samia amesema Tanzania na Namibia zina historia ya pekee kutokana na mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Namibia, ambapo wakati wa harakati hizo Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kupitia Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Afrika (OAU Liberation Committee) kusaidia nchi za kusini mwa Afrika kupata uhuru.
Ameongeza kuwa uhusiano huo umejengwa pia na viongozi waasisi wa mataifa hayo, akiwataja Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Dkt. Sam Nujoma wa Namibia, ambao waliweka msingi wa urafiki na ushirikiano uliopo hadi sasa.
Rais Samia amesema licha ya uhusiano huo wa kihistoria, Tanzania na Namibia bado zina safari ya kuhakikisha ushirikiano wa kisiasa na kidiplomasia unaendana na maendeleo ya kiuchumi, akibainisha kuwa biashara kati ya nchi hizo bado iko chini na inahitaji kuimarishwa zaidi.
Amesema katika mazungumzo yao wamekubaliana kukuza biashara na uwekezaji, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kimkakati kama mafuta na gesi, madini, usalama, uchumi wa buluu, kilimo, mifugo na utalii.
Ameeleza kuwa Tanzania na Namibia zina fursa kubwa katika sekta ya uchumi wa buluu kutokana na kuwa na rasilimali nyingi za bahari, hivyo nchi hizo zitabadilishana uzoefu na kutumia fursa hizo kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.
Kwa upande wa mafuta na gesi, Rais Samia amesema nchi hizo zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kupitia mashirika yao ya kitaifa kwa kubadilishana maarifa, teknolojia na kujenga uwezo ili kunufaika na rasilimali hizo.
Aidha, amesema wamezungumzia kuimarisha ushirikiano katika sekta ya mifugo, ambapo Namibia imepiga hatua kubwa na Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya mifugo barani Afrika, huku pia wakijadili kuanzishwa kwa safari za ndege kati ya nchi hizo mbili ili kukuza biashara na utalii.
Kwa upande wake, Rais wa Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah amesema Tanzania imekuwa nyumbani kwa Namibia katika kipindi cha mapambano ya ukombozi, akitoa shukrani kwa msaada mkubwa wa kisiasa, kidiplomasia na kiutendaji uliotolewa na Tanzania wakati wa harakati za kupata uhuru.
Amesema ziara yake imelenga kubadilisha mshikamano wa muda mrefu wa kisiasa kuwa ushirikiano wa vitendo katika uchumi, biashara na uwekezaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vya kiutawala ili kurahisisha mtiririko wa bidhaa na mitaji kati ya mataifa hayo.
Ameongeza kuwa nchi hizo zimekubaliana kuhakikisha makubaliano yao yanafanyiwa kazi kwa vitendo kupitia mifumo ya ushirikiano baina ya nchi mbili, hususan Tume ya Pamoja ya Ushirikiano, huku mawaziri na wataalamu wakipewa jukumu la kuongeza kasi ya utekelezaji.
Katika kuimarisha uhusiano huo, viongozi hao wameshuhudia kutiwa saini kwa mikataba minne ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo ulinzi, biashara na uwekezaji, kukuza biashara za viwanda vidogo na vya kati, pamoja na maeneo mengine ya ushirikiano yatakayofungua fursa mpya kwa wananchi wa Tanzania na Namibia.

