Na Timothy Mwakyenda – MAELEZO
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari amesema uandikishaji na uboreshaji wa Anwani za Makazi nchini umechangia kwa kiasi kikubwa kukuza biashara mtandaoni kwa kuwasaidia wafanyabiashara kutambua kwa urahisi maeneo wanakoishi wateja wao.
Dkt. Bakari ameyasema hayo leo Februari 5, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kilichopo jijini Dar es Salaam wakati akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Hamis Abdullah katika ufunguzi wa Kongamano la Anwani za Makazi pamoja na Maonesho ya Teknolojia ya huduma za Posta.
Amesema kuwa, uwepo wa anuani za makazi umeimarisha uchumi wa kidijitali, umeimarisha usalama wa jamii na kuongeza pato la taifa kupitia urahisishwaji wa huduma mbalimbali za kibiashara na kijamii.
“Mfumo mzima wa uchumi wa kidijitali unahitaji uwepo wa anwani za makazi ili uweze kufanya kazi ipasavyo. Ndiyo maana leo viongozi wa Serikali za Mitaa wapo hapa ili kutusaidia kuboresha anwani zilizopo na kuanzisha anwani katika maeneo ambayo hayajafikiwa.
Wiki hii tutahamasisha wananchi kujua umuhimu wa anwani za makazi na kushiriki katika kuziweka,” amesema Dkt. Bakari.
Ameongeza kwa kufafanua kuwa, itakuwa ngumu huduma za kiusalama kuwafikia wananchi kwa ufanisi bila kuwa na anwani sahihi za makazi zinazotambua mahali watu wanapoishi.
Vile vile, huduma za afya na biashara mtandaoni zinategemea kwa kiasi kikubwa anwani za makazi ili kuwafikia walengwa kwa haraka na kwa usahihi.
Kwa upande wake, Ferdinand Kabyemela aliyemwakilisha Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania amesema, utekelezaji wa anwani za makazi unaenda sambamba na ufanisi wa huduma za posta nchini.
Amesema ili Shirika la Posta liweze kuwafikia wateja wake kwa haraka na kwa ufanisi, ni lazima kuwe na anwani sahihi za makazi zitakazorahisisha utambuzi wa maeneo ya wateja.
Ameongeza kuwa, wafanyabiashara wa mtandaoni watanufaika zaidi kwa kuwa wataweza kufikisha bidhaa kwa wateja kwa wakati na kwa gharama nafuu kupitia matumizi sahihi ya anuani za makazi.





