……..
Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameonesha kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika elimu na mafunzo ya ufundi stadi, baada ya ziara yake katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chemba leo, tarehe 5 Februari, 2026.
Ziara hiyo imelenga kujionea maendeleo ya ujenzi na uendeshaji wa vyuo vya VETA katika kila wilaya, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Ilani ya CCM.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Nchimbi amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuboresha elimu ya ufundi stadi kwa kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kwa lengo la kuongeza tija na kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
“Nimekagua karakana za mafunzo na nimefurahishwa sana na kazi inayoendelea, maelezo niliyopita yanaonesha utekelezaji wa dhati wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuboresha elimu nchini,” amesema Dkt. Nchimbi.
Ameongeza kuwa amevutiwa na nidhamu, umakini na ubunifu wa wanafunzi, hali inayoakisi ubora wa mafunzo wanayopata.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ilinunua vifaa na mitambo ya kisasa ya kufundishia yenye thamani ya Sh. Bilioni 8.4, ambavyo vilisambazwa katika vyuo 63 vya ufundi stadi nchini, ikiwemo Chuo cha Ufundi Stadi cha Chemba.
Akitoa maelezo zaidi, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema vifaa vilivyopo katika vyuo vya VETA ni vya kisasa na vinawawezesha vijana kujifunza teknolojia za viwandani na zisizo za viwandani kulingana na mahitaji ya soko la ajira.
“Tunaishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kupata vifaa vya kisasa. Kupitia vifaa hivi, vijana wetu wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira,” amesema CPA Kasore.





