Mkurugenzi Mkuu wa TAEC ,Profesa Najat Kassim Mohamed akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea miradi hiyo
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha , WAKALA wa kimataifa wa Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) umetembelea Makao Makuu ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) yaliyopo jijini Arusha kwa lengo la kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na wakala huo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea Tume hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC ,Profesa Najat Kassim Mohamed amesema kuwa ,ziara hiyo imelenga kuangalia kwa karibu mradi wa uboreshaji wa mbegu bora kwa kutumia teknolojia ya nyuklia, mradi unaolenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kuhimili mabadiliko ya tabianchi, pamoja na mradi wa ujenzi wa maabara ya kisasa itakayoongeza uwezo wa nchi katika tafiti za kisayansi na uchunguzi wa kitaalamu.
Aidha, ugeni huo umetembelea mradi wa uanzishaji wa vifaa vya irradiator, vinavyotumika kuhifadhi ubora wa mazao na bidhaa mbalimbali kwa kuzuia wadudu na kuongeza muda wa matumizi.
“sambamba na mradi mkubwa wa sekta ya afya unaolenga kuongeza vituo vya matibabu ya saratani nchini kutoka vituo vinne vya sasa hadi kufikia vituo sita.”amesema Mkurugenzi wa TAEC .
Profesa amesema kuwa ,ziara hiyo imelenga kutathmini maendeleo ya miradi hiyo ili kuwezesha IAEA kuendelea kutoa ufadhili na msaada wa kitaalamu, sambamba na kuimarisha ushirikiano katika matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo ya kilimo, afya na sayansi nchini Tanzania.
Uongozi wa TAEC umeeleza kuwa miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kutumia sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu.
“ushirikiano na IAEA umeleta manufaa makubwa kwa wananchi kupitia ongezeko la uzalishaji wa chakula na kuboreshwa kwa huduma za matibabu ya saratani.”amesema Profesa .
Aidha Profesa Najat amefurahishwa na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kuuleza kuwa miradi inatekelezwa vizuri na kwa wakati na kusema endapo utakamilika italeta manufaa makubwa sana kwa wananchi kwa ujumla.
Aidha ugeni huo umeambatana na Kaimu Mkurugenzi wa idara ya ushirikiano wa kiufundi Afrika ,Gashaw Wolde pamoja na Afisa wa usimamizi wa programu Afrika, Azza Kashlan .




