NA DENIS MLOWE,IRINGA
Msemaji wa Familia, Mwalimu Solomoni Mkangwa akizungumza na wanahabari alisema kuwa Shughuli ya kumuaga mzee Ngajilo inatarajiwa kuanza saa 3:00 asubuhi katika uwanja wa ikiongozwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, viongozi wa chama, ndugu, jamaa na marafiki.
Miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria ni Mwenyekiti wa Wazazi Taifa, Fadhili Maganya, Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano Mhandisi Yusuph Masauni, pamoja na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndugu Gerson Msigwa, atakayewakilisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mzee Fabian Ngajilo ni baba mzazi wa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, ndugu Ngajilo, na pia baba mzazi wa mfanyabiashara maarufu nchini, Fred Vunjabei, mmiliki wa maduka ya Vunjabei yaliyosambaa maeneo mbalimbali nchini, na mdau muhimu wa maendeleo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali.
Wasifu na Maisha Ya Mzee Ngajilo
Kwa mujibu wa waliomfahamu, Mzee Ngajilo amekumbukwa kama mtu mwenye upendo, ukarimu na uchapa kazi. Grayson Yona Manonge, Katibu wa Wazazi Mkoa wa Iringa, ameeleza kuwa marehemu alikuwa mtu wa kujitolea sana kusaidia wageni na jamii bila kuchoka.
“Nilikuwa ninamfahamu vizuri, alikuwa mcheshi, mkarimu na mwenye moyo wa kusaidia. Mara nyingi tulipopata wageni ama mahali pa kuwapokea, mzee alitoa msaada bila kusita,” amesema.
Naye Bernard Clement Ngoro, ambaye amekuwa fundi na msaidizi wa marehemu kwa zaidi ya miaka 13, ameeleza kwa uchungu siku za mwisho za maisha ya mzee Ngajilo.
Amesema walikuwa pamoja kwenye safari ya kwenda Njombe, ambapo mzee alifanya shughuli zake, lakini baadaye afya yake ilianza kubadilika baada ya kiwango cha sukari kupanda hadi 26.
Ameeleza kuwa licha ya juhudi za kumkimbiza hospitali na usaidizi kutoka kwa ndugu na viongozi, ikiwemo mawasiliano na mbunge wa Iringa Mjini, hali ya mzee iliendelea kuwa tete na hatimaye alipoteza maisha akiwa ICU katika Hospitali ya Mkoa wa Niombe.
Safari ya Mwisho
Baada ya kuagwa Uwanja wa Samora kesho mwili wa Mzee Ngajilo utapelekwa Kata ya Mseke, umbali wa takribani kilomita 10 kutoka Manispaa ya Iringa, katika Kijiji cha Ubwachanya, ambako atapumzishwa katika makazi yake ya milele.
Shughuli zinaongozwa na MC Mwalimu Mkangwa, ambaye ametoa mwito kwa wananchi wote wa Iringa na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kutoa heshima za mwisho kwa mzee wao mpendwa.





