Na Sophia Kingimali.
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matoleo ya kidato cha nne huku Ufaulu wa wanafunzi umeendelea kuimarika na umefikia asilimia 94.98, ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.61 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Akitangaza matokeo hayo, ya mtihani uliofanyika Novemba 17, 2025, leo Januari 31, 2026 jijini Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, amesema jumla ya watahiniwa 595,810 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 318,910 sawa na asilimia 53.53 na wavulana 276,900 sawa na asilimia 46.47.
Amesema kati ya watahiniwa hao, 526,620 wamefaulu kwa kupata madaraja ya I, II, III na IV, huku ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu ukiwa ni wanafunzi 255,404 sawa na asilimia 46.1, idadi ambayo imeongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Profesa Mohamed ameeleza kuwa jumla ya wanafunzi 569,883 walifanya mtihani huo wakiwa wamesajiliwa katika shule 5,864, huku watahiniwa wa kujitegemea wakiwa 25,927 waliosajiliwa katika vituo 813 nchini.
Kwa upande wa jinsia, amesema kati ya waliofaulu, wasichana ni 278,108 sawa na asilimia 94.26 ya wasichana wote wenye matokeo, huku wavulana wakiwa 248,512 sawa na asilimia 95.79 ya wavulana wote wenye matokeo.
Hata hivyo, NECTA imesema wanafunzi 77 wamefutiwa matokeo yao baada ya kubainika kuandika lugha ya matusi kwenye skripti za mitihani na wengine kujihusisha na udanganyifu, ambapo kati yao 47 walitoka katika vituo vya mtihani na 30 kutoka shule mbalimbali.




