Serikali imesema maboresho yanayoendelea kufanyika katika usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka nchini yanakusudia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi katika sekta mbalimbali.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika banda la Idara hiyo lililopo kwenye maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa umma 2026 Juni 22,2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bwana Filiman Msiangi amesema taarifa sahihi na zinazopatikana kwa wakati ni msingi muhimu wa kufanya maamuzi yanayogusa maisha ya wananchi.

Amesema idara hiyo ina jukumu la kuhakikisha nyaraka zote zinazozalishwa katika taasisi za umma zinahifadhiwa katika mifumo salama na yenye kuzingatia matakwa ya sheria na sera za nchi.Kwa mujibu wa Bwana Msiangi, maeneo ya ardhi, afya, elimu na maji yanahitaji mifumo imara ya kumbukumbu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuondoa changamoto zinazotokana na upotevu wa taarifa muhimu.

Amesema serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya mfumo wa masijala mtandao (e-office) ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ameeleza kuwa hatua hiyo pia inatekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mifumo ya serikali inasomana na kurahisisha utendaji kazi katika taasisi mbalimbali za umma.