Na OWM – TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amazielekeza Halmashauri za wilaya ya Mkinga, Mafia, Mpwapwa, Kondoa, Chamwino, Mtwara, Mtama na Manispaa ya Kigamboni kutumia Bilioni 5.2 za programu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (Local Climate Adaptive Facility-LoCAL) kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuwanufaisha wananchi.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo Juni 22, 2026 jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI, mara baada ya kukabidhiwa hundi yenye thamani ya Bilioni 5.2 za kitanzania na Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) Bw. Pradeep Kurukulasuriya, ambalo linafadhili utelelezaji wa programu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (LoCAL).
“Katumieni fedha hizi kama zilivyoanishwa kwenye maelekezo ya mradi huu, kama ambavyo tumefanya vizuri katika utekelezaji wa awamu ya kwanza kwenye halmashauri za Chamwino, Kondoa na Mpwapwa,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe ameeleza kuwa, utekelezaji mzuri wa awamu ya kwanza ya mradi wa LoCAL katika Halmashauri hizo umewezesha kupatikana kwa mradi mpya wa SCALE wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambao unaotekelezwa katika halmashauri 54 nchini.
Katika kuongeza ufanisi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Prof. Shemdoe ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kuongeza kuwa milango ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ipo wazi kwa mdau yeyote mwenye nia ya kuwasaidia wananchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, Diplomasia ya Uchumi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndio inayofungua milango ya wadau mbalimbali kuja kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mratibu wa Mradi wa LoCAL Wilaya ya Kondoa Bw. Laurence Robert Mogela amesema Halmashauri ya Kondoa imepokea dola za kimarekani 149,043 kwa ajili utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo, utakaotekelezwa kwenye Kata ya Bumbuta kupitia kilimo cha kisasa kitakachoimarisha usalama wa chakula.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Wilaya ya Chamwino Bi. Elizabeth Solwa amesema wananchi wengi wa Wilaya ya Chamwino watanufaika na fedha za mradi wa LoCAL kwani wilaya itapokea milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya mradi huo katika kata mbili za Mtamalo na Mvumi Makulu.
Naye, Mratibu wa Mradi wa LoCAL Wilaya ya Mpwapwa Bw. Issa Abdallah Sepanja, amesema wilaya ya Mpwapwa imepokea Shilingi Milioni 491 kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa LoCAL ambazo zitatumika katika vijiji vya Godegode na Kitati kuchimba visima vya umwagiliaji na kujenga mfereji wa umwagiliaji wenye urefu wa mita 1200.

