Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mheshimiwa Patrick Adkin Mwalunenge, leo tarehe 31 Januari 2026 ameongoza zoezi la usafi katika Soko la Mwanjelwa, jijini Mbeya, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha usafi na utunzaji wa mazingira katika maeneo ya biashara.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mheshimiwa Mwalunenge amewataka wananchi, hususan wafanyabiashara wa soko hilo, kuweka mazoea ya mara kwa mara ya kufanya usafi katika maeneo yao ya kazi badala ya kusubiri siku maalum au maagizo kutoka kwa viongozi.
Amesema mazingira safi husaidia kulinda afya za wananchi, kuzuia magonjwa ya mlipuko na pia kuboresha mwonekano wa soko, jambo linalovutia wateja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara.
“Usafi ni jukumu la kila mmoja wetu. Tukijenga utamaduni wa kufanya usafi kila siku, tutapunguza magonjwa na kufanya soko letu liwe salama na lenye kuvutia,” amesema Mwalunenge.
Zoezi hilo limehusisha viongozi wa serikali za mitaa, wafanyabiashara pamoja na wananchi, ambapo walishiriki kwa pamoja kufanya usafi wa maeneo ya soko, kuondoa taka na kusafisha mifereji ya maji.
Mwisho, Mbunge huyo amesisitiza kuwa ataendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha usafi na mazingira bora vinaendelezwa katika masoko na maeneo mengine ya biashara ndani ya Jimbo la Mbeya Mjini.




