Na John Bukuku – Dar es Salaam
Kufungwa kwa mafanikio makubwa kwa mauzo ya awali ya hisa (IPO) ya iTrust EAC Large Cap Exchange Traded Fund (ETF) kumeanza kufungua ukurasa mpya katika maendeleo ya masoko ya mitaji nchini Tanzania, huku kuorodheshwa kwake katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kukitarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wawekezaji wadogo na wakubwa
Kuorodheshwa kwa ETF hiyo kunamaanisha kuwa mwekezaji iTRUST ETF YAANZA BIASHARA DSE, FURSA KWA WAWEKEZAJI WADOGO wa kawaida wa Kitanzania ataweza kununua na kuuza bidhaa hiyo moja kwa moja sokoni kama ilivyo kwa hisa za kawaida, hata kama hakushiriki katika kipindi cha IPO. Hatua hii inalenga kupanua wigo wa uwekezaji kwa wananchi wengi zaidi, hususan wale wanaoanza safari ya uwekezaji katika masoko ya mitaji.
Soko la Hisa la Dar es Salaam linasema limejipanga kukabiliana na ongezeko la wawekezaji wadogo kupitia mifumo ya biashara ya kielektroniki, programu za elimu ya kifedha na ushirikiano wa karibu na wadau wa sekta ya masoko ya mitaji. DSE inaeleza kuwa uzoefu uliopatikana wakati wa IPO hii utatumika kuboresha uanzishwaji wa ETF nyingine na bidhaa mpya za kifedha siku zijazo.
Kwa upande wake, iTrust imeeleza kuwa mfuko huo umeundwa kutoa fursa kwa wawekezaji wa kawaida kushiriki katika ukuaji wa kampuni kubwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wawekezaji wanatarajiwa kunufaika na ukuaji wa mtaji wa muda mrefu pamoja na mapato yatokanayo na gawio, kulingana na utendaji wa masoko na kampuni zinazounda mfuko huo.
Hata hivyo, iTrust imebainisha kuwa kama ilivyo kwa uwekezaji mwingine wowote wa masoko ya mitaji, ETF hiyo inaambatana na hatari mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya soko, athari za kubadilika kwa thamani ya fedha za kigeni pamoja na hatari za kisiasa na kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki. Hatari hizo zinasimamiwa kwa kutumia mkakati wa usambazaji wa uwekezaji, ufuatiliaji wa karibu wa masoko na kuzingatia kwa ukamilifu mkakati wa uwekezaji uliotangazwa kwa umma.
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia kwa karibu utendaji wa ETF hiyo baada ya kuanza kufanya biashara sokoni, kwa lengo la kuhakikisha mfuko unazingatia malengo na viwango vya hatari vilivyobainishwa. CMSA inaeleza kuwa mifumo ya udhibiti na uwazi wa taarifa imewekwa ili kuwalinda wawekezaji wadogo dhidi ya upotevu usio wa lazima, hata katika nyakati za msukosuko wa kifedha au kushuka kwa soko.
DSE na iTrust pia zimeeleza kuwa mwekezaji wa kawaida hahitaji mtaji mkubwa kuanza kununua au kuuza ETF hiyo, jambo linalolenga kukuza ujumuishi wa kifedha. Aidha, kutokana na mafanikio ya IPO iliyovuka lengo kwa zaidi ya asilimia 540, wadau hao wameweka mikakati ya kuhakikisha kunakuwepo ukwasi wa kutosha sokoni ili wawekezaji waweze kufanya miamala bila kusababisha mabadiliko makubwa ya bei.
Kuhusu uwazi, iTrust kwa kushirikiana na CMSA imeahidi kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu uwekezaji halisi wa mfuko, gharama na ada pamoja na utendaji wake kwa ujumla, ili wawekezaji waweze kufanya maamuzi sahihi.
Kwa ujumla, wadau wa masoko ya mitaji wanaeleza kuwa mafanikio na utendaji wa ETF hii yatapimwa kwa kuangalia kiwango cha biashara sokoni, idadi ya wawekezaji wanaoshiriki, faida za muda mrefu kwa wawekezaji na mchango wake katika kuimarisha uthabiti wa soko la mitaji nchini Tanzania, wakitaja kuorodheshwa kwa iTrust EAC Large Cap ETF kuwa hatua muhimu katika kuendeleza uwekezaji wa kisasa na jumuishi kwa Watanzania.

