Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM- TAMISEMI) anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali chini ya Mradi wa TACTIC kuzingatia viwango vya ubora vilivyoainishwa katika mikataba yao.
Mhandisi Mativila ametoa agizo hilo Mei 29,2026 wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya miundombinu inayotekelezwa na TACTIC katika mkoa wa Mara, ambapo amesisitiza kuwa ubora wa kazi ni jambo lisilopaswa kufanyiwa mzaha.
“Katika ziara hii, moja ya mambo muhimu tunayoyaangalia ni ubora wa miradi kwa kuzingatia maelezo yaliyopo kwenye mikataba, hivyo wakandarasi wote mnapaswa kuhakikisha mnatekeleza kazi kwa viwango vilivyokubaliwa,” amesema Mhandisi Mativila.
Ameeleza kuwa wakandarasi wanaposaini mikataba ya utekelezaji wa miradi, wanakuwa wamekubali kutekeleza kazi kwa ubora unaotakiwa, hivyo ni wajibu wao kujisimamia na kuhakikisha wanazingatia masharti yote ya mikataba bila kushurutishwa.
Aidha, Mhandisi Mativila amesema kuwa utekelezaji wa miradi kwa ubora ni sehemu ya kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akisisitiza umuhimu wa kujenga miradi yenye viwango bora ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Mativila amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Mradi wa TACTIC, ikiwemo ujenzi wa soko, jengo la Ofisi ya TARURA pamoja na Stendi ya Bweli iliyopo mkoani humo.

