Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Homera akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wapya kabla ya kukabidhi magodolo kwa watumishi hao.
Na Muhidin Amri,Namtumbo
WAZIRI wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mkoani Ruvuma Dkt Juma Zuberi Homera, ametoa jumla ya magodoro 222 kwa watumishi wapya 202 walioajiriwa na Serikali na kupelekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo na magodoro 13 kwa ajili ya watumishi 13 wanaotarajiwa kuajiriwa na akiba magodoro 7, ikiwa ni jitihada za kuwajengea mazingira rafiki ya kazi na maisha.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magodoro hayo iliyofanyika katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Waziri Homera Homera alisema, msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Samia Suluhu Hassan kutekeleza ahadi yake kuajiri watumishi katika sekta mbalimbali kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi ndani ya siku 100 za uongozi wake.
Dkt. Homera amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo kwa ajili ya kuleta maendeleo ya Jimbo la Namtumbo na Taifa kwa ujumla.
Aidha, amewaomba viongozi wa Chama na katika Wilaya ya Namtumbo kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi kwa watumishi hao ikiwemo kuwapatia maeneo ya kilimo ili kuboresha ustawi wao wa maisha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Francis Pili,amempongeza Dkt Homera kwa jitihada anazofanya za kuboresha maisha ya watumishi na wananchi wa Jimbo la Namtumbo kwani hatua hiyo itawezesha watumishi wapya kufanya kazi kwa bidii katika kuwatumikia wananchi ambao wanamatumaini makubwa na Serikali yao ya awamu ya sita.
Pili,amewaasa watumishi wapya kwenda kufanya kazi na kuondoa dhana potofu kwamba Namtumbo sio sehemu rafiki kwa watumishi kutokana na mazingira yake kwa sababu Serikali inaendelea kuboresha mazingira mazuri kwa watumishi wake ikiwemo ujenzi wa barabara,huduma ya majisafi na salama,afya na nishati ya umeme.
Amewasisitiza watumishi hao kuhusu suala la uwajibikaji zaidi kwa namna ambavyo kila mmoja anavyotakiwa kujitoa wakati wa kutekeleza majukumua yake pamoja na changamoto watakazokutananazo watakapofika sehemu zao za kazi.
Akizungumzia umuhimu wa kutatua kero za watumishi Pili alisema,ni muhimu kwa wakuu wa idara na vitengo kutenga muda maaluma wa kukutana na kusikiliza kero na matatizo ya watumishi walio chini yao na kutafuta ufumbuzi wake.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Namtumbo Musa Mumina,amemshukuru Dkt Homera kwa msaada huo kwani utachochea morali na ufanisi wa watumishi wapya katika utekelezaji wa majukumu yao huku wakiongeza kuwa ni mara ya kwanza kutolewa kwa motisha hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya watumishi waliokabidhiwa magodoro hayo wamemshukuru Dkt. Homera kwa kuwajali na kuahidi kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kutoa huduma bora kwa wananchi wa Wilaya ya Namtumbo.





