Na John Walter -Manyara
Shirika la maendeleo la ECLAT Development Foundation, kupitia Mkurugenzi wake Bw. Peter Toima, limetangaza kuanza kwa awamu ya pili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Merekwa iliyopo Kata ya Dirma, Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara.
Bw. Toima amesema ujenzi huo unatarajiwa kuanza rasmi mapema mwezi Februari, huku shule hiyo ikipangwa kukabidhiwa serikalini tarehe 24 Novemba, 2026. Jumla ya shilingi 286,302,200 zinatarajiwa kutumika katika awamu ya kwanza na ya pili ya ujenzi.
Shule ikikamilika itakuwa na ofisi za walimu, madarasa, madawati, samani, jiko pamoja na vyoo kwa walimu na wanafunzi, hatua itakayoboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa jamii za pembezoni, hususan jamii za wafugaji.
Amesema ECLAT hufanya kazi kwa vitendo zaidi kuliko maneno, akisisitiza kuwa hawavumi lakini wapo, wakifanya kazi kwa ajili ya wananchi bila kujitamba.
Ameongeza kuwa shirika hilo linafanya kazi katika mikoa sita na zaidi ya wilaya tisa, ambapo tayari zimeshajengwa takribani shule 60 za msingi, pamoja na ujenzi wa shule za sekondari.
Mbunge wa Jimbo la Hanang’, Mheshimiwa Asia Halamga, ameishukuru ECLAT kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa elimu, akieleza kuwa ujenzi wa shule hiyo ni msaada mkubwa kwa watoto wa maeneo ya mbali.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Bw. George Bajuta, ameahidi ushirikiano wa karibu na shirika la ECLAT ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora.





