Na John Walter-Babati
Mkurugenzi wa Shirika la ECLAT Development Foundation ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Ndugu Peter Toima, amefanya mazungumzo na Diwani wa Kata ya Magugu Mheshimiwa Stanley Charles pamoja na kamati ya maendeleo ya kata (WDC) kwa lengo la kujadili ushirikiano wa pamoja katika kuharakisha maendeleo ya kata hiyo.
Jambo kubwa lililojadiliwa katika kikao hicho ni dhamira ya Shirika la ECLAT Development Foundation kuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika Kata ya Magugu, hususan kwenye sekta ya elimu na miundombinu ya huduma za kijamii.
Toima alieleza kuwa shirika hilo lipo tayari kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa pamoja na wananchi katika kutatua changamoto zinazowakabili, hasa katika uboreshaji wa miundombinu ya shule na mabweni ya wanafunzi wa shule za sekondari.
Katika ziara hiyo, Toima alitembelea maeneo mbalimbali yenye changamoto ya miundombinu ya huduma za shule na mabweni, ambapo alijionea hali halisi ya uchakavu wa majengo pamoja na mahitaji makubwa ya upanuzi wa miundombinu hiyo ili kukidhi ongezeko la wanafunzi.
Aidha, alitembelea vijiji vitano (5) ndani ya Kata ya Magugu na kufanya mazungumzo na viongozi pamoja na wadau wa maendeleo, ambapo kwa pamoja wamekubaliana kuanza kushirikiana rasmi na Shirika la ECLAT Development Foundation ili kuleta maendeleo ya haraka na endelevu katika kata hiyo.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Diwani wa Kata ya Magugu Mheshimiwa Stanley Charles alisema kuwa mazungumzo hayo ni hatua muhimu ya mwanzo wa ushirikiano mkubwa ambao utakuwa ni mwarobaini wa changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya elimu katika kata hiyo.
Alibainisha kuwa ushirikiano huo unatarajiwa kusaidia kutatua kero ya umbali mrefu wa wanafunzi kufuata shule, uchakavu wa miundombinu ya elimu pamoja na kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika shule chache zilizopo.
“Kwa sasa tuna shule za msingi zenye wanafunzi zaidi ya 1,000, hali ambayo inaathiri ubora wa elimu.
Ushirikiano huu utatusaidia kupunguza msongamano, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, pamoja na kusogeza huduma za elimu karibu zaidi na wananchi,” alisema Mheshimiwa Stanley Charles.
Mazungumzo hayo yameelezwa kuwa ni mwanzo wa hatua mpya ya ushirikiano kati ya Shirika la ECLAT Development Foundation na Kata ya Magugu, yenye lengo la kuleta mabadiliko chanya na maendeleo ya kweli kwa wananchi kupitia miradi ya kijamii na kielimu.





