Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Jumla ya vijana 5,746 wamechaguliwa kujiunga na mafunzo ya uanagenzi ya miezi nane katika vyuo 47 vilivyopo nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, Januari 16, 2026, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Waziri Sangu amesema kuwa Novemba 5, 2025, Serikali ilitoa tangazo kwa vijana kuomba kushiriki mafunzo ya ufundi stadi, ambapo jumla ya vijana 20,247 waliwasilisha maombi.
Amesema kuwa baada ya kukamilika kwa mchakato wa usaili, vijana 5,746 walichaguliwa kujiunga na mafunzo hayo ya uanagenzi.
Aidha, amebainisha kuwa mafunzo hayo yatatekelezwa kwa kipindi cha miezi nane katika fani mbalimbali ikiwemo upishi, ushonaji na ubunifu wa mitindo.
Amesema kuwa mafunzo hayo yatatolewa katika vyuo 47 vilivyochaguliwa baada ya vyuo 103 kuomba kushirikiana na Serikali.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itawalipia ada ya mafunzo kiasi cha shilingi 500,000 kwa kila kijana atakayeshiriki mafunzo hayo ya uanagenzi
Aidha, amebainisha kuwa fani zitakazofundishwa ni pamoja na ubunifu wa mitindo na ushonaji nguo, ufundi bomba, uashi, useremala, uchomeleaji na uungaji vyuma, upakaji rangi na maandishi ya alama, upishi, ufundi magari na mitambo, umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa magari, huduma za hoteli na utalii pamoja na ufundi vyuma.
Aidha, amebainisha kuwa baada ya wahitimu kukamilisha mafunzo yao, serikali imeweka mazingira wezeshi ya kuwaunganisha na fursa za mikopo na mitaji ili kuwawezesha kuanzisha biashara na kampuni ndogo ndogo pamoja na kujiajiri.




