Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano – TEHAMA (ICTC) , Dkt. Nkundwe Mwasaga akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 16, 2026 jijini Dar es Salaam.
…………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC) inatarajia kuwakutanisha wadau wa sekta ya TEHAMA kutoka ndani na nje ya nchi kupitia Kongamano la Tisa lenye lengo la kujadili masuala muhimu, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, hususan katika mapinduzi ya kidijitali (Digital Transformation). Kongamano hilo litafanyika kwa siku tano kuanzia Januari 19 hadi 23, mwaka huu, katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 16, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema kongamano hilo linatoa fursa kwa wadau wa TEHAMA nchini kukutana na mataifa mbalimbali kwa ajili ya kujadiliana masuala muhimu, ikiwemo mapinduzi ya kidijitali, ambayo yatasaidia kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 ya kufikia uchumi wa trilioni moja ya dola za Marekani (one trillion US dollars).
Dkt. Mwasaga amesema kuwa dira hiyo imebainisha mapinduzi ya kidijitali kuwa ni dereva muhimu atakayoipeleka dira hiyo kwa kasi, hivyo kongamano hilo linatoa fursa ya kuwasikiliza wataalamu wa ndani na nje ya nchi, makampuni, sekta ya umma na binafsi, ambao watajadiliana kwa pamoja.
Amebainisha kuwa mapinduzi ya kidijitali yana nguzo tano, ikiwemo ujuzi wa kidijitali unaomsaidia mtu kujua kutumia mifumo mbalimbali, pamoja na wataalamu wa ngazi ya kati wanaosaidia kutatua changamoto zinazojitokeza katika mifumo hiyo.
Amesema nguzo nyingine ni uwepo wa watu wenye ujuzi wa juu wa kidijitali wanaosaidia kutengeneza mifumo mahususi, hususan inayotumia akili unde (AI), ambayo usaidia kufikisha huduma mbalimbali kwa jamii kwa ufanisi mkubwa.
“Katika kongamano hili pia tutajadiliana kuhusu usalama wa mitandao, ulinzi wa faragha na taarifa binafsi, umuhimu wa huduma za mawasiliano, uchumi wa kidijitali, utafiti, ubunifu na ujasiriamali,” amesema Dkt. Mwasaga.
Amesisitiza kuwa kongamano hilo ni mahususi kwa ajili ya kujadili Dira ya mwaka 2050 na kujiandaa kwa wataalamu wa TEHAMA pamoja na wananchi wote wanaotumia mitandao katika shughuli zao za kila siku, jambo litakalosaidia kuanza utekelezaji wa dira hiyo kuanzia Julai 1, 2026 kwa ufanisi mkubwa.
Amesema siku ya kwanza ya kongamano hilo kutakuwa na mada ya wanawake na TEHAMA, ambapo watajadili mafanikio, changamoto zilizopo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kufikia uchumi jumuishi.
Siku ya pili itahusu vijana, huku akieleza kuwa katika siku mbili za mwanzo kila mtu anaweza kushiriki. “Siku ya tatu, nne na tano zitawahusisha wataalamu wa TEHAMA pekee, hivyo si kila mtu ataruhusiwa kushiriki,” amesema Dkt. Mwasaga.
Aidha, Dkt. Mwasaga amesema katika uchumi wa kidijitali kila mtu anapaswa kuhusika na kupata fursa ya matumizi ya teknolojia za kidijitali kupitia huduma mbalimbali za mawasiliano.




