Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula akieleza jambo wakati wa mkutano na Watumishi wa Afya katika Hospitali ya Mirembe Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa utumishi na rasiriamali watu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Bi Deodatha Makani akisisitiza jambo wakati wa mkutano na Watumishi wa Afya katika Hospitali ya Mirembe Jijini Dodoma.
Watumishi wa Hospitali ya Mirembe wakifuatilia kwa makini neno kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula wakati wa kikao chake na Watumishi wao cha kusikiliza changamoto zinazowakabili katika Hospitali hiyo.
Afisa Muuguzi na Mwenyekiti wa kamati ya kufuatilia Maendeleo ya Hospitali ya Mirembe Bw. Davis Silvester Mwantela akitoa maoni mbele ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula (hayupo kwenye picha) wakati wa mkutano na Watumishi wa Afya katika Hospitali ya Mirembe Jijini Dodoma.
…………………………………………………………………………………………………………
Na WAMJW-DOM
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo yaJamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula amewataka watumishi na uongozi wa Hospitali ya Mirembe kuhakikisha wanatembea pamoja kwa kudumisha ushirikiano baina yao ili kuleta mabadiliko chanya ikiwemo kuboresha huduma zitolewazo na kuboresha stahiki za watumishi katika hospitali hiyo.
Dkt. Chaula amesema hayo jana wakati alipofanya ziara ya kutembelea Hospitali ya Mirembe na kufanya mazungumzo na Watumishi ili kujadiliana namna gani watatatua changamoto walizonazo katika maeneo yao ya kazi.
“Tunatakiwa kukaa pamoja na tutembee pamoja wakati wote, ili kuleta mabadiliko katika Hospitali na taasisi yetu, tuache kulalamika maana sisi sote tulio hapa ndio Serikali yenyewe”. Amesema Dkt. Chaula.
Kwa upande mwingine, Dkt. Chaula ameagiza uongozi wa Hospitali ya Mirembe kuwa wabunifu kwa kuhakikisha wanasimamia miradi yao vizuri hali itakayosaidia kuongeza makusanyo ya mapato na kupelekea kuboresha huduma za Afya na stahiki za Watumishi katika hospitali hiyo.
“Hospitali inatakiwa iwe ya mfano hivyo mnatakiwa kuongeza jitihada na ubunifu katika utendaji wenu, ikiwemo usimamizi mzuri wa miradi, tunataka kuona mabadiliko ili kuweza kusonga mbele”. Amesema Dkt. Chaula.
Aidha, Dkt. Chaula ameagiza maboresho katika maabara, huku akiahidi kurudi baada ya wiki moja ili kuona maboresho yaliyofanywa, ikiwa ni sehemu ya usimamizi na ufuatiliaji wa maboresho ya huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.
Mbali na hayo, Dkt. Chaula ametoa wito kwa watumishi katika hospitali hiyo kwenda katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kujifunza baadhi ya mbinu na ubunifu wanaoutumia katika kuendesha baadhi ya idara zao ili kuleta mabadiliko ya haraka ikiwemo katika suala la ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande mwingine, Dkt. Chaula ametoa wito kwa Watumishi katika Hospitali hiyo kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kutenda haki kwa kutoa huduma kwa usawa kwa wagonjwa wote katika maeneo ya kazi.