Bw. Ganga Ben Mlipano Meneja Msaidizi Dawati la Malalamiko ya Wateja na Mabenki na Taasisi za Fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akitoa mada kuhusu Dawati hilo na namna linavyofanya kazi katika semina ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari inayofanyika kwenye tawi la BoT jijini Arusha.
Baadhi ya waaandishi wa habari wakimsikiliza Bw. Ganga Ben Mlipano Meneja Msaidizi Dawati la Malalamiko ya Wateja na Mabenki na Taasisi za Fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati akitoa mada kuhusu Dawati hilo na namna linavyofanya kazi katika semina hiyo.
………………………………………………
Kuanzishwa kwa kanuni mpya za kusaidia kutatua malalamiko ya mteja (Bank Of Tanzania Financial Consumer Protection Regulation) za mwaka 2019 kumesaidia kupunguza muda wa malalamiko mengi na ukomo wa kiwango kilichokuwa kimewekwa kwa wateja ambacho kilikuwa ni shilingi milioni 15.000.000 lakini kwa sasa ni zaidi ya fedha hizo.
Wateja wengi kwenye mabenki walikutana na mikataba yenye lugha ngumu ambayo iliwachanganya na wengi walichukua mikopo bila kujua faida na athari za mikopo hiyo jambo ambalo liliwaletea usumbufu mwingi.
Bw. Ganga Ben Mlipano Meneja Msaidizi Dawati la Malalamiko ya Wateja na Mabenki na Taasisi za Fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoa mada kuhusu Dawati hilo katika semina ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari inayofanyika kwenye tawi la BoT jijini Arusha .
Bw. Ganga amesema ilikuwa inachukua muda mrefu sana kuwarudishia wateja hati zao za dhamana ya mkopo wakati wanapokuwa wamemaliza kulipa mikopo yao walikuwa wamechukua.
Ameongeza kuwa malalamiko mengi yalikuwa yakichukua muda mrefu kutatuliwa tofauti na sasa ambapo muda huo umepungua sana ,Kwa mujibu wa kanuni hizo zimeweka muda mfupi zaidi wa kutatuliwa kwa malalamiko ambao ni masaa sita, Masaa nane , Wiki moja ,Wiki Mbili na mengine ambayo ni magumu yatachukua siku 45.
Ameongeza kuwa kanuni hizi zina ainisha kuwa benki inatakiwa kumweleza wazi mteja kwanini amenyimwa mkopo, Mteja akishamaliza mkopo wake lazima arudishiwe hati yake aliyoiweka kama dhamana haraka na kuhakikisha kwamba kama mteja amenyimwa mkopo lazima aambiwe ndani ya siku saba.
Benki pia inatakiwa kumweleza wazi mteja kuhusu mkopo anaochukua na athari zake ili kumuondolea usumbufu wa kurudi benki mara nyingi akifuatilia mkopo wake na kujua kama atapewa au hatapewa ikiwa ni pamoja na kujua faida na athari za mkopo huo wakati atakapokuwa amechukua.
Amesema Sekta ya kibenki ni muhumi sana kwa uchumi hivyo lengo la BoT ni kuhakikisha wateja wanahudumiwa vizuri na kwa haraka ili waendelee kuweka fedha zao benki badala ya kuweka nyumbani ili wakirudi nyumbani wawaambie na wengine kuhusu umuhimu wa kuweka fedha zao benki na ubora wa huduma zinazotolewa .
Benki Kuu ya Tanzania ilianzisha Dawati la Malalamiko kwa ajili ya kutatua migogoro ya wateja Aprili mosi mwaka 2015 na kutoka wakati huo mpaka sasa limetatua migogoro mingi jambo ambalo limesaidia kupunguza matatizo kuhusu huduma za mabenki kwa wateja wake.