Na John Bukuku – Dar es Salaam
Programu ya Viongozi Chipukizi inayoratibiwa na Uongizi Institute inaendelea kufanyika jijini Dar es Salaam na kwa njia ya mtandao, ikiwa na lengo la kuwaandaa viongozi wa baadaye kuendana na mabadiliko ya kiutendaji katika taasisi mbalimbali.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mhe. Regina Qwaray, amesema kuwa ni muhimu kwa viongozi kupokea matokeo hasi kutoka kwa wananchi wanaowaongoza na kuyatumia kama fursa ya kuboresha utendaji ili kuwaridhisha wananchi.
Ameyasema hayo Desemba 11, 2025 jijini Dar es Salaam. Aidha, amesema kuwa matokeo yanayotolewa na watu anaowaongoza yanaweza kumsaidia kiongozi kupanga na kubuni mikakati mipya ya kuboresha utendaji wake. Amebainisha kuwa kukamilika kwa programu hiyo kutaleta matokeo chanya na kuwasaidia viongozi chipukizi kubadilika na kuendana na wakati.
Pia, amesema kuwa vijana wengi wanapoingia katika nafasi mbalimbali huja na mawazo mapya, hivyo ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi kuhusu mabadiliko ya kiutendaji unaweza kusababisha mgongano wa kimaslahi. Amekazia kuwa programu kama hizi zinapaswa kuwa endelevu ili kuwasaidia vijana na viongozi chipukizi kufuata mabadiliko ya dunia ya sasa.
Aidha, amesema kuwa kiongozi anatakiwa kutambua uwezo wake, udhaifu wake na kupanga namna ya kutatua changamoto zake. Ameongeza kuwa kiongozi anapaswa kuinua wengine waliopo chini yake kwa kuwaandaa kuwa viongozi wa baadaye.
Pia, amebainisha kuwa kukubali matokeo ya pande zote mbili—chanya na hasi—kunamsaidia kiongozi kujua namna anavyochukuliwa na watu anaowaongoza pamoja na kupata tathmini ya utendaji wake.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Uongizi Institute, Bw. Kadari Singo, amesema kuwa lengo la kuanzisha programu ya Viongozi Chipukizi ni kuwaandaa washiriki mapema kabla hawajafikia ngazi za juu za kiuongozi, na amebainisha kuwa programu hiyo inaanzia Tanzania.
Aidha, ameeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia viongozi chipukizi kutambua vipaji vyao wakiwa bado wadogo na kuepuka kujifunza kupitia makosa. Amesema kuwa programu inahusisha mafunzo ya mawasiliano, mabadiliko na masuala mengine muhimu.
Aidha, amesema kuwa mafunzo hayo yanadumu kwa miezi sita (6) na kusisitiza kuwa dunia ya sasa inahitaji kuzungumza uhalisia kutokana na kuwepo kwa matamanio halisi na yasiyo halisi. Amesema vijana wanaandaliwa kuifahamu dunia ya teknolojia wanayoielekea.
Aidha, amebainisha kuwa vigezo vya kupata mafunzo hayo ni pamoja na kijana aliyejiandaa kuwa kiongozi na anayeonyesha utayari wake.





