Ubao wa Uwanja wa Benjamin Mkapa umehitimisha dakika 90 kwa kusoma Simba SC 0–2 Azam FC, matokeo yaliyowapa matajiri wa Dar pointi tatu muhimu katika Mzizima Derby.

Timu zote mbili ziliingia uwanjani zikiwa na kiu ya ushindi, lakini mwisho wa mchezo Azam FC ndio waliotoka na tabasamu baada ya kuonesha umakini mkubwa katika kipindi cha pili.

Mabao yote mawili yalipatikana katika dakika za lala–salama, wakati mchezo ukikaribia kutamatika.

Jephte Kitambala alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 81 baada ya kuuwahi mpira ndani ya eneo la hatari na kumtungua kipa wa Simba.

Idd Nado akaongeza bao la pili dakika ya 89, akimaliza vyema shambulizi la kasi lililowapoteza mabeki wa Simba.

Huu unakuwa mchezo wa kwanza kwa Simba SC kupoteza uwanjani katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2025/26, huku Azam FC wakiondoka Mkapa wakiwa wameweka rekodi muhimu dhidi ya mpinzani wao mkubwa jijini Dar es Salaam.