NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Iringa Mjini., Fadhili Ngajilo amewaahidi wananchi wa Kata ya Kwakilosa atashughulikia kila kero kwa kushirikiana na diwani wa kata mara baada ya kuwa na ziara ya mtaa kwa mtaa katika kata hiyo ikiwa ni mwendelezo wa kutembelea wananchi kusikiliza kero zao.
Alisema kuwa aliwaahidi wananchi wakati wa kampeni atakuwa mstari wa mbele kuwasikiliza zaidi wao katika changamoto mbalimbali ambazo zinazikumba kata zao na yeye kuzichukua na kuzifanyia kazi ambapo zile ndogo ndogo anazimaliza hapo hapo na zile kubwa anazichukua kwa utekelezaji zaidi.
Kwenye ziara hiyo Mbunge Ngajilo alitumia muda mwingi kuwasikiliza wananch zaidi wenye kero na kutoa msaada kwa. Changamoto ambazo aliziahidi wakati wa kampeni ikiwemo msaada wa vifaa vya ujenzi wa choo katika Kilabu cha Pombe za Kienyeji cha Kijiweni
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo wa mabati, saruji, mbao na sink za matundu matano ya choo yenye thamani ya sh milioni 1 Ngajilo alisema kuwa msaada huo ametoa ikiwa ni ahadi aliyowapa wakati wa kampeni ili wawe na choo bora.
Licha ya msaada wa vifaa hivyo Ngajilo alikabidhi kiasi cha laki mbili ili kisaidie ujenzi wa choo hicho ambapo ametoa wiki moja kiweze kukamilika.
Aidha Ngajilo aliweza kuzungumza na kada mbalimbali wakiwemo wamiliki wa karakana za magari ‘gerejj’ na kuchukua changamoto zao ambapo zilizokuwa kubwa amezichukua kwa ajili ya utekelezaji zaidi.
Wananchi wengine waliotoa kero zao ni mama lishe wa stend ya Dabaga , bodaboda na wananchi wa kawaida ambao walizungumzia kero ya miundo mbinu mibovu katika stendi hiyo na mbunge kuwaahidi kuyatatua changamoto hizo.
Kwa upande wa kijiwe cha bodaboda cha Frelimo aliwaahidi kuwakarabatia kijiwe chao ambapo wamekuwa wakikumbwa na changamoto wakati wa mvua na kipindi cha jua kali.
Vile vile alizungumzia kuhusu eneo la kiuchumi linaloongoza kwa kuwa na gareji nyingi kukumbwa na changamoto za miundo mbinu ambapo amesema kuwa watashughulikia changamoto hizo.
Akizungumzia kuhusu michezo Ngajilo alieema kuwa atahakikisha mashindano ya Vunjabei Cup yanaendelea na yatarudi kwa jina la Ngajilo Cup na kutakuwa na bonanza la michezo Kuanzia Disemba 24 hadi Disemba 31 ambapo kutakuwa na michezo kila aina.
Katika suala la michezo watoto wenye vipaji waliomba kuwe na ligi ya watoto na Ngajilo kutoa wito kwa walimu wakuu wajiandae kwani ataanzisha ligi ya watoto ndani ya jimbo la Iringa.





