Mgombea ubunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salome Makamba akizugumza kwenye. mkutano uliofanyika u wanna wa Magufuli mjini Kahama
…………
NA JOHN BUKUKI- KAHAMA
Mgombea ubunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salome Makamba, amesema kuwa miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta mabadiliko makubwa katika kuinua hadhi ya mwanamke na mtoto wa kike nchini.
Akizungumza Oktoba 11, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kahama mkoani Shinyanga, Makamba alisema kuwa kila mwanamke anayezaa mtoto wa kike sasa anajivunia kutokana na mafanikio ya Dkt. Samia katika kuwatetea wanawake na kuhakikisha wanapewa nafasi muhimu katika jamii.
Aidha, Makamba alibainisha kuwa dhamira ya Dkt. Samia katika kulinda heshima ya wanawake imepelekea kupungua kwa visa vya mimba na ndoa za utotoni. Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, idadi ya wasichana waliodahiliwa mashuleni imeongezeka maradufu kutokana na juhudi hizo.
Amesema licha ya changamoto zinazowakabili wanawake na vijana, Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia imeweka mazingira wezeshi kwa wote kupitia sera, sheria na kanuni zinazolenga kutoa fursa sawa katika elimu, ajira na biashara.
Makamba aliongeza kuwa Dkt. Samia ameonesha utafiti na uelewa wa kipekee kuhusu changamoto za wafanyabiashara wadogo, ambapo amepanga kutoa shilingi bilioni 200 kama mitaji ya kuimarisha biashara ndogondogo nchini, ikiwemo zile zinazomilikiwa na wanawake na vijana.
“Mama yetu Samia amegundua kuwa wafanyabiashara wengi hawana mitaji. Ndani ya siku 100 tangu atangazwe Rais, aliahidi kutoa bilioni 200 kwa ajili ya mitaji hiyo. Hii ni fursa kubwa kwa vijana wa Kahama na Shinyanga,” amesema Makamba.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali imepanga kutoa ajira kwa vijana zaidi ya elfu saba sambamba na kuendeleza miundombinu ya elimu ili kutoa nafasi zaidi kwa vijana waliohitimu kupata ajira stahiki.
Makamba amewataka wananchi wa Kahama na Shinyanga kusimama imara na kumpigia kura za kishindo Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema kuwa ni mwanamke shupavu mwenye maono ya kuijenga Tanzania yenye usawa wa kijinsia na maendeleo jumuishi.
Amesema kuwa wananchi wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza wamejipanga kumpa “send-off ya heshima” kabla ya kufunga kampeni zake, wakionesha dhamira ya dhati ya kuunga mkono juhudi za Dkt. Samia katika ujenzi wa taifa.
“Nawaomba wanasiasa wenzangu, vijana, wanawake na wanaume, tusimame pamoja kumpigia kura mama yetu Samia. Ni Rais aliyeleta matumaini mapya kwa wanawake, vijana na taifa kwa ujumla,” amesema Makamba.