Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ikungi (kushoto) Ally Mwanga na Makamu wake Stephano Missai wakifuatilia matukio ya kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi, Justise Kijazi akizungumza kwenye kikao cha baraza hilo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ikungi Ally Mwanga akizungumza.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, (aliyevaa shati ya bluu katikati) Edward Mpogolo, na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye moja ya tukio la kikao hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akitoa zawadi kwa Watendaji ambao Kata zao zimefanya vizuri zaidi katika ukusanyaji wa mapato ndani ya Halmashauri.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akitoa zawadi kwa Watendaji ambao Kata zao zimefanya vizuri zaidi katika ukusanyaji wa mapato ndani ya Halmashauri.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akitoa zawadi kwa Watendaji ambao Kata zao zimefanya vizuri zaidi katika ukusanyaji wa mapato ndani ya Halmashauri.
Mwekahazina wa Halmashauri ya Ikungi, akisoma taarifa mbele ya Baraza la Madiwani.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu akizungumza kwenye kikao hicho.
Na Mwandishi Wetu
WATAALAMU wa kilimo wameagizwa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wananchi waweze kulima mazao ambayo yatawapatia chakula na kuepukana na baa la njaa kutokana na mashamba mengi kusombwa na maji yanayotokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha mkoani Singida.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Mwanga alitoa wito huo juzi wakati alipokuwa akifungua kikao cha baraza la madiwani Wilayani humo ambapo alitoa taarifa za uharibifu mkubwa uliotokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha kwenye Wilaya hiyo ikiwemo mazao yaliyolimwa na wananchi kusombwa na maji huku mifugo yao ikikosa malisho baada ya maeneo mengi kujaa maji.
Kutokana na hali hiyo Mwenyekiti huyo aliwataka wataalamu wa kilimo wa Wilaya hiyo kutoa ushauri wa kitaalamu haraka iwezekanavyo ili kutafuta mazao mbadala yatakayofidia yale yaliyosombwa na maji tayari kwa lengo la kuwasaidia wananchi kuepukana na tishio la ukosefu wa chakula,huku akimuomba mkuu wa Wilaya hiyo Edward Mpogolo kuwatafutia eneo la malisho ya mifugo wananchi ili kunusuru mifugo yao isije ikafa kwa kukosa malisho
“Mkuu wetu wa Wilaya tunakuomba kama inawezekana pembezoni mwa eneo la hifadhi yetu ya misitu sio ndani kuwaazima kwa muda wananchi kwa ajili ya malisho ya mifugo,maeneo waliyokuwa wanayategemea yamejaa maji hivyo hakuna malisho.” alisema mwenyekiti.
Aidha Mkuu wa Wilaya hiyo Mpogolo alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kutoa taarifa za maafa yaliyotokea kwa nyakati tofauti Wilayani humo ikiwa ni pamoja na zaidi ya watu 20 kufariki dunia,Nyumba zaidi ya 400 kuvunjwa na mifugo mingi kufa,hivyo alitumia fursa hiyo kuzitaka kamati za maafa kutoa taarifa mapema ili kuweza kuchukua hatua za kuwasaidia watu wanapokutana na majanga hayo na kuwaomba viongozi kushirikiana kwa pamoja kwa kupeana taarifa vinapotokea viashiria vya maafa ili hatua za kuzuia maafa hayo ziweze kuchukuliwa
Pia Mpogolo alimpongeza mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa usimamizi thabiti wa mapato na kuifanya Halmashauri kuwa ya mfano kwa mkoa na hata kitaifa,licha ya kuwa na vyanzo kama zilivyo Halmashauri zingine.
“Kwakweli ndugu yangu na rafiki yangu Kijazi nakupongeza kwakusimamia suala la ukusanyaji wa mapato, umeipaisha Wilaya yetu.” alisema Mpogolo.
Katika hatua nyingine Halmashauri hiyo kupitia Baraza hilo ilitoa tuzo kwa watendaji wa kata zilizofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha miezi mitatu kama sehemu ya kutoa motisha kwa watendaji hao.
Lengo ni kuijenga Halmashauri ya ikungi, ambapo katika makusanyo hayo kata zilizopata zawadi ni kata ya Makilawa ambayo ilikusanya sh milioni 85,265,000/= na kupewa zawadi ya pesa taslimu Sh.250,000/= kata ya pili ni kata ya Iglansoni ilikusanya sh.milioni 69,466,200 na kupewa zawadi ya pesa taslimu sh.200,000/= na kata ya tatu ni kata ya Iyumbu yenyewe ilikusanya Sh.milioni 69,098,000 na kupata zawadi ya Sh.150,000/=.
Mwenyekiti huyo wa baraza Mwanga alimpongeza mkurugenzi wa Halmashauri hiyo bwana Justis kijazi kwa kutoa motisha kwa watendaji hao,huku akimtaka kusimamia na kuhakikisha madeni wanayodaiwa baadhi ya watendaji wa kata yanalipwa na kuwaomba madiwani hao kuendelea kushirikiana na watendaji hao na kusimamia ukusanyaji wa mapato kwenye kata zao.
Huku Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi Ccm Wilaya hiyo Mika Likapakapa aliwataka Viongozi wa halmashauri hiyo wakiwemo watendaji wa kata kuwa waadilifu katika utendaji wao wa kazi kwani chama hakitamvumilia kiongozi asiye mwadilifu,na kuishauri Halmashauri hiyo kuongeza vyanzo vya mapato kuliko kutegemea chanzo kimoja pekee,huku akiitaka kuboresha vyanzo vyake vya mapato kwa kutoa mfano wa maeneo ya minada kuwa mazingira yake hayako vizuri,hakuna vyoo licha ya kukusanya mapato.
“Ili upate mapato ni lazima uviboreshe vyanzo vyako kwa kuweka mazingira vizuri,siku moja nienda pale mnada wa ikungi na viongozi wakubwa niliona aibu,hakuna choo,boresheni vyanzo vyenu vya mapato.” alisema Likapakapa.
Halmashauri hiyo ya Ikungi inatajwa kuwa ni miongoni mwa Halmashauri nchini zilizofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ambapo kimkoa ni halmashauri ya kwanza kati ya halmashauri saba za mkoa huo.