Home Mchanganyiko WAGANGA WA TIBA ASILI/MBADALA FUATENI SHERIA-DKT. CHAULA

WAGANGA WA TIBA ASILI/MBADALA FUATENI SHERIA-DKT. CHAULA

0

Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akiongea na waandishi wa habari

Wanafunzi wa sekondari walioshiriki kongamano la wajasiriamali na upimaji wa afya

Watoto wakimsikiliza Katibu Mkuu(hayupo pichani)

……………………………………………………………………………………………..

Na.Catherine Sungura, Chato

Waganja wa Tiba asili na tiba mbadala wote nchini, wametakiwa kufanya kazi zao kwa kufuata Sheria, kanuni, taratibu zilizowekwa na Serikali .

Hayo yamesemwa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Idara kuu afya Dkt. Zainab Chaula alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua kongamano la wajasiriamali lililoandaliwa na Chama cha Wanataaluma Waadventista Tanzania (ATAPE).

Dkt. Chaula alisema hadi sasa Tanzania hakuna mgonjwa Corona wala dawa iliyothibitishwa kuwa na uwezo wa kutibu ugonjwa huo hapa nchini.

“Tanzania hakuna mgonjwa wa Corona wala dawa iliyothibitishwa kuwa na uwezo wa kutibu ugonjwa huo, kwa yule ambaye ametangaza kwamba ana dawa, Serikali imechukua hatua”.

Aidha, aliwataka waganga wa tiba asili/mbadala wote wazingatie kufanya kazi zao kwa mujibu wa matakwa ya Serikali, “wizara kupitia kitengo cha tiba asili na tiba mbadala pamoja na msajili wa baraza hilo wametoa sheria na taratibu za kujisajili,lazima wajisajili, lakini wakifanya kazi bila kufuata ile misingi, bila kutii mamlaka iliyopo madarakani, hatutasita kumchukulia hatua yeyote atakayekiuka,” alisisitiza.

Dkt. Chaula aliwahimiza wananchi kuendelea kufuata kanuni za afya na maelekezo yanayotolewa na wataalamu ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko ambayo yanaendelea kuripotiwa katika maeneo mengine duniani kama vile Ebola na Corona.

Aliwahimiza wazazi kuwakatia watoto wadogo na wale wanafunzi waliopo sekondari na vyuoni bima ya afya ili waweze kupata huduma za matibabu popote nchini wanapokuwa wagonjwa.

“Nawaona wanafunzi wa sekondari hapa ni vyema mzazi akakata bima ile ya elfu hamsini na mia nne(50,400) ili iweze kuwasaidia kupata matibabu mahali popote na kuwapunguzia mzigo wazazi pindi mtoto anapougua”.