Na Sophia Kingimali.
Afisa mradi wa NOURISH kutoka katika shirika la RECODA Salome James,ameweka wazi mafanikio ya mradi huo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wakulima kujifunza kwa vitendo kanuni bora za kilimo chenye tija kinachostahimili mabadiliko ya tabia nchi kupitia mashamba darasa, pamoja na kuwaunganisha wakulima wadogo na makampuni yanayozalisha na kusambaza pembejeo bora za kilimo.
Hayo ameyasema wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Endanoga wilaya ya Babati wakati akifunga Maadhimisho ya wakulima wa NOURISH yaliochukua wiki nne kwa nyakati tofauti katika halmashauri za wilaya 10 Tanzania, ambapo mradi huo ulianza utekelezaji wake wilayani humo mwaka 2024 na hadi sasa
“Mpaka sasa tumefanikiwa kuanzisha vikundi vya kilimo 75 vikiwa na jumla ya wanachama 2,346, mashamba darasa 57, kusambaza Mbegu za viazi lishe kwa lengo la kuzalisha mbegu kwenye ngazi ya kata ambapo jumla ya pingili 40,000 zimekwishatolewa. “amesema Salome.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa wilaya ya Babati Khalfan Matipula amepongeza mradi wa NOURISH kwa mradi kuwaongezea ujuzi wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wamekua chachu katika kutoa elimu ya afya na lishe katika jamii zetu ili kupunguza tatizo la utapiamlo haswa udumavu kwa Watoto na kusisitiza wakulima washiriki wa mradi kuwa chachu ya maendeleo kwa kutekeleza kwenye kaya zao yale waliyojifunza na kushiriki katika vikundi na wataalamu wa kilimo na wakulima viongozi (lead farmers) pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
“Maisha bora yanapatikana kwa kila mmoja kufanya kazi kwa bidii na kwa kutumia utaalamu. Nishauri tena wataalamu wa ugani hakikisheni mnawajibika kuleta maendeleo hasa kwa kwenda na hili wimbi la mradi huu ambao umeonyesha njia ya kweli ya maendeleo vijijini.” amesema Matipula.
Mradi wa NOURISH wilayani Babati unatekelezwa katika vijiji 42 vilivyoko katika kata 10 ambapo utekelezaji wa mradi huu, mashirika wabia wamekuwa wakitumia maafisa ugani, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na wakulima viongozi wa ngazi ya kijiji ambao walichaguliwa na serikali za vijiji na kupewa mafunzo juu ya utekelezaji wa kazi zao kabla ya kuanza kufanya kazi za mradi.
Mradi wa NOURISH Tanzania (Kuwawezesha Wakulima Wadogo kwa Usalama wa Chakula na Ustahimilivu wa Tabianchi) ni mradi wa miaka mitano (2024-2028) unaolenga kufanikisha usalama wa chakula unaozingatia ustahimilivu wa tabianchi kwa watu 168,000, wakiwemo wakulima wadogo, biashara ndogo na za kati (MSMEs), na vikundi vya wakulima katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Rukwa, Singida, na Songwe. Kwa kuzingatia minyororo minne ya thamani yenye uwezo mkubwa (mtama, alizeti, maharage, na mboga mboga),
Lakini pia.mradi unashughulikia changamoto za usalama wa chakula kwa wakulima wadogo kupitia njia tatu kuu za mafanikio ambazo ni Kuongeza uzalishaji kupitia mafunzo ya kilimo kinachozingatia tabianchi, upatikanaji wa pembejeo bora, na rasilimali za kifedha.
Pia,Kuimarisha masoko ya chakula kwa kushirikisha wadau wa biashara, kutumia suluhisho za kidijitali, na kuwawezesha wakulima wadogo na MSMEs na Kuboresha matumizi ya rasilimali za kaya kwa kuhamasisha mlo wenye lishe bora, bajeti ya chakula cha kaya, na kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kaya.
Maadhimisho ya wakulima wa NOURISH yamefikia tamati katika wilaya ya Babati na kufikia wakulima maelfu kupitia elimu ya kilimo chenye tija na lishe bora. Wilaya ya Babati imehitimisha kilele cha maadhimisho haya ambayo yalianza mnamo ukingoni mwa mwezi wa nne kwa kuleta pamoja wakulima na wadau mbali mbali wa kilimo kujifunza na kusherehekea mafanikio ya mradi wa NOURISH wilayani humo.
Mradi unafadhiliwa na Shirika la maendeleo la Norway (Norad) na kutekelezwa kwa ushirikiano wa SNV, Farm Africa, T-MARC, RECODA, na MIICO