Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mfanyabiashara maarufu na mdau mkubwa wa maendeleo katika Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, ametoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ili kuhakikisha wanatumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.
Koola alitoa kauli hiyo jana, Mei 17, 2025, aliposhiriki zoezi la uboreshaji wa taarifa zake katika kituo cha uandikishaji kilichopo Mahakamani, kijiji cha Kiruweni, kitongoji cha Kiruweni Kati, kata ya Mwika Kusini, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro — eneo ambalo pia ni nyumbani kwake.
Akizungumza baada ya kujiandikisha, Koola alisema kuwa ni wajibu wa kila mwananchi, hususan vijana, kujitokeza katika zoezi hilo muhimu ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao.
“Ni muhimu kwa kila kijana kuhakikisha yupo kwenye daftari la wapiga kura. Kura yako ni sauti yako. Tusikubali kupoteza haki hii ya msingi kwa uzembe au kutojali,” alisema Koola.
Koola pia aliwataka vijana wa bodaboda na makundi mengine ya vijana ambao kwa kiasi kikubwa huathiriwa na maamuzi ya kisiasa, kuhakikisha wanatumia fursa hii kujiandikisha na kuwa sehemu ya mabadiliko wanayoyataka.
Aidha, alisisitiza kuwa zoezi hilo si la kisiasa, bali ni la kijamii na kimaendeleo kwa sababu linaamua mustakabali wa nchi. Alisema kuwa viongozi bora hupatikana kupitia kura, hivyo ni muhimu kila mwananchi kuchukua hatua ya awali ya kuhakikisha anastahili kupiga kura.
“Mabadiliko tunayoyapigania hayawezi kuja bila hatua za msingi kama hizi. Na hatua ya kwanza kabisa ni kujiandikisha,” aliongeza.
Koola alihitimisha kwa kutoa wito kwa viongozi wa maeneo mbalimbali kuendelea kuhamasisha wananchi, hasa vijana, kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uandikishaji kama njia ya kulinda misingi ya demokrasia.