Wenyeviti wa vijiji vinavyozunguka Pori la Akiba la Grumeti, Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara, wameiomba Grumeti Fund kuweka uzio wa umeme ili kutenganisha eneo la hifadhi na makazi ya wananchi. Lengo la ombi hilo ni kuzuia mauaji ya watu na mifugo pamoja na uharibifu wa mazao unaofanywa na wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yao.
Wenyeviti hao walitoa kauli hiyo baada ya kutembelea vijiji vya Bonchugu, Kazi, Rwamchanga, Nisekee, na Parknyigoti, ambavyo tayari vimenufaika na uwekaji wa uzio huo kwa ushirikiano kati ya Grumeti Fund na Serikali. Walisema uwepo wa uzio umewezesha vijiji hivyo kuepuka uvamizi wa wanyamapori na kuboresha maisha ya wakazi wa maeneo hayo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mashujaa, Ezekiel Kahabi, alisema kuwa kuna upotoshaji kuhusu uzio huo, ambapo baadhi ya watu wanadai kuwa unasababisha madhara kwa watoto. Hata hivyo, alisisitiza kuwa madai hayo si ya kweli na kutoa mfano wa wananchi wa Serengeti ambao tayari wamenufaika na uzio huo.
“Nilizungumza na baadhi ya wananchi wa Serengeti, ambao wamewekewa uzio, na mambo yao yako vizuri. Wanalima mazao yao, hata miwa ambayo ni kivutio kwa tembo, lakini haijaharibiwa kwa sababu ya uzio huu. Pia, watoto wanakwenda shule bila kuhofia kukutana na tembo au simba. Tunaomba Serikali iruhusu jambo hili lifanyike kwetu pia, maana tunateseka sana,” alisema Kahabi.
Wenyeviti hao waliongeza kuwa uwekaji wa uzio huo kwa upande wa Bunda utapunguza mzigo kwa Serikali wa kulipa kifuta machozi kwa waathirika wa wanyamapori. Walisema kiasi cha kifuta machozi kinachotolewa kwa wananchi wanaopoteza mazao au mifugo ni kidogo sana na hakiwezi kukidhi mahitaji yao, hasa ikilinganishwa na thamani ya mazao yanayoharibiwa na tembo au mifugo inayouawa na simba.
Mwisho, viongozi hao waliomba hatua za haraka zichukuliwe ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao, huku wakisisitiza kuwa uzio wa umeme ndio suluhisho la kudumu kwa changamoto hiyo.